USHUHUDA ALIOUTOA DADA DEBORA RWECHUNGURA:-

Namshukuru Mungu kwa wema wake na matendo yake makuu.. Kwanza namshukuru kwa kuniookoa na kwa kuniponya magonjwa ambayo yalikuwa yananiandama mara kwa mara. Na pia kaniponya na mitego mingi tu ya ibilisi na kwa kweli nimeendelea kumuona Mungu katika maeneo mbalimbali ya maisha.

Tangu siku nilipookoka tu, maisha yangu yalikutana na kipindi kigumu sana ambacho wengine wanasema ni mapito na kwa ujumla katika kipindi hiki nimemuona Mungu akisimama na kunipigania. Maana katika kipindi hicho kila njia ile ambayo huwa inaingiza riziki kwa mwanadamu, kwangu ni kama ilifungwa.na nikaanza kuhangaika maana hata pale nilipokuwa nikifanya kazi niliachishwa. Hivyo nikaanza kuzunguka huku na huko nikitafuta namna ya kuishi maana kama yalivyo maisha ya mjini kila kitu ni fedha, kama kwa mfano nyumba unayolala na matumizi mengineyo yote yanahitaji pesa, lakini kila nililojaribu kulifanya halikufanikiwa, nami nikajiuliza je nitaishije Mungu wangu ?

Katika kipindi hicho mimi nilikuwa bado mchanga kiroho na sikuwa najua la kufanya katika maisha yangu ya wokovu. Hata hivyo namshukuru Roho mtakatifu wa Mungu ambaye aliniongoza na kunileta katika Unity Christian Fellowship hapa Tumaini Shule ya Msingi, maana kumbe hapo ndipo palipokuwa na uponyaji wangu.

Kusema kweli kama si Yesu ambaye aliniokoa na kunipeleka katika fellowship sijui ningekuwa wapi! Maana wengi katika fellowship ni mashahidi wa hali yote iliyokuwa imenikuta. Sijui ningekuwa wapi, na labda ningeshatoweka hata katika uso wa nchi au ningekuwepo na sijui ningekuwa mtu wa aina gani!.

Nakumbuka katika kipindi hicho cha mapito magumu ilikuwapo semina ambayo mtumishi mmoja wa Mungu alitufundisha jambo fulani juu ya Mungu alivyowatoa wana wa Israel Misri maana aliwaona wana wa Israel wameteseka sana miaka 400 katika nchi ya Misri katika utumwa na hivyo akakusudia kuwatoa huko na kuwapeleka Kanani, na ajabu ni kwamba Mungu hakuwatoa huko kwa njia ya mkato ili awapeleke Kanani katika nchi ya maziwa na asali aliyokuwa amewaahidi bali aliwapitisha jangwani miaka 40 na wale waliokuwa wamestahimili ndiyo waliofika Kanani.

Semina hiyo ilinikuta katika hali mbaya na ya kuchoka kabisa ingawa haikuwa hali ya kukata tamaa lakini bado ilikuwa hali ya kuchoka kabisa. Hata hivyo baada ya semina nilisikia kutiwa moyo na kuona labda ile semina ilikuwa imenilenga mimi. Nikaona inawezekana watu wa Mungu, Mungu anapokuwa ametuokoa kutoka katika utumwa wa ibilisi na kutuahidia kutupa mema ya nchi kumbe kuna kipindi cha kupita jangwani na hapo nikagundua kumbe na mimi niko katika kipindi cha kupita jangwani na nitafika Kanani. Namshukuru Mungu kwamba hata katika kipindi hicho cha kupita Jangwani Mungu hakunitupa bali aliendelea kunishika na kwa uaminifu wake kabisa aliendelea kunisaidia na kuniimarisha ili nisianguke.

Napenda nikutie moyo wewe ndugu yangu yamkini wewe pia umekutana na mambo mabaya na magumu katika wokovu wako, na inawezekana unapita katika shida na majaribu, mimi napenda nikutie moyo mpendwa kwamba usikate tamaa na mwisho ukawa kama wale walioanguka jangwani, maana katika kipindi hicho cha jangwani ndipo wengi waliookoka wanapoanguka. Siku ya kukuvusha Mungu na kukupeleka Kanani ipo.

Namshukuru Mungu ambaye kanipigania katika kipindi hicho na nikaweza kuvuka na kwa sasa najiona kama niko kanaani.

RUDI UKURASA WA KWANZA

RUDI MWANZO WA UKURASA HUU