USHUHUDA ULIOTOLEWA NA BI HAPPY

Napenda kumshukuru Mungu kwa wema wake wa ajabu maana kaniponya nguvu za giza zilizoniijia kwa njia ya pepo la mahaba. Mara nyingi nilipokuwa nikilala usiku nilikuwa naota kuwa nina mwanaume nimelala naye nikifanya naye tendo la ndoa. Hali hii ilinipata hata kama mume wangu alikuwa hayupo kwani bado nilijikuta nikiwa katika hali ya kusikia nimelala na mwanaume na nafanya naye tendo la ndoa.

Hali yote hii iliendelea kunitokea hata nilipokuwa nimeshaokoka. Nilijaribu kufunga na kuomba mara kwa mara lakini hali hiyo iliendelea.

Nyumbani kwetu kwa kujua kuwa bado sijapata mimba ingawa niko katika ndoa kwa miaka miwili walinishauri nikafanye kafara kwa mizimu ya kwetu wakiamini kuwa hilo ndilo kiini cha tatizo la kutozaa kwangu na pia hii hali ya kufanya tendo la ndoa na mapepo. Nililipinga jambo hili kwa sababu niliamini kuwa kwa kuwa nimeokoka, Bwana Yesu yupo na atanipigania na nitapata ushindi. Ni ajabu kwamba bado hali hii iliendelea kunisumbua. Baadaye nilikwenda kwenye mkutano wa injili wa mtumishi wa Mungu Moses Kulola na kuombewa shida yangu hii lakini hali hii haikuacha kuendelea kunisumbua.

Siku moja nilimsimulia mpendwa mmoja mateso ninayoyapata, na alinishauri nimuone na kumshirikisha mtumishi wa Mungu Johannes Kasimbazi na kumuelezea msiba unaonikuta. Nilimfuata mtumishi wa Mungu Johanes Kasimbazi na kumuelezea hali yote inayonikuta na aliniwekea mikono na kuniombea na kunipa ushauri. Tangu siku hiyo sijapata tena shida iliyokuwa ikinipata na wala lile pepo halijarudi tena kufanya tendo la ndoa na mimi.

Najua Yesu kaniponya na nampa sifa na utukufu kwa matendo yake makuu ya miujiza anayoyafanya katika maisha yetu.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

RUDI UKURASA WA KWANZA

RUDI MWANZO WA UKURASA HUU