USHUHUDA

Mnamo mwaka 1988 nilikuwa mtu ninayejali masuala ya dini yangu na sikuamini habari za wokovu.

Ilitokea katika mwaka huo wa 1988 watu fulani walikuja kwangu ili kunihubiri injili ya upendo wa Bwana Yesu, nami niliwasikiliza na nilipoona sina haja ya kubishana nao ingawa nilikuwa sihitaji kuokoka, bado niliona ni vema niwalidhishe kwa kukubaliana nao kila takwa lao ili kufupisha mjadala wa kuwabishia kwamba wokovu haupo. Na kwa sababu hiyo ingawa halikuwa kusudi la moyo wangu kuokoka kila waliponiuliza kama nilitaka kuokoka niliwakubalia kwamba ndio nataka kuokoka. Na walipotaka nipige magoti ili waniongoze sala ya toba nilikubaliana nao, na walipoomba kuniombea nilikubaliana nao ingawa hakika ndani ya moyo wangu sikuwa nahitaji kuokoka. Nia yangu ilikuwa waondoke na kutoendelea kunibughudhi na shuhuda zao za wokovu. Na baada ya yote hayo niliendelea na kwenda kanisani kwetu na maisha yangu ya kawaida ambayo hakika hayakuwa na mabadiliko yoyote. Niliendelea kuishi nikijua moyoni mwangu hakika kwamba sijaokoka ingawa niliwahi kuongozwa sala ya toba. Na ilipofika mwaka 1999 niliugua kifua na kikawa kikinisumbua sana. Nilikwenda hospitali kuu ya Mkoa wa Kagera pale Bukoba na nikachunguzwa na kupewa dawa nyingi tu. Lakini bado hazikuwa msaada wowote katika maumivu niliyokuwa nayo. Hivyo ilibidi nikachunguzwe kwa kupigwa X-Ray lakini bado nilionekana kutokuwa na mabadiliko yoyote katika kupata uponyaji. Nikarudia kuchunguzwa tena kwa x ray kwa mara ya pili lakini bado ikaonekana sina tatizo lolote. Hapo ofisini kwangu waliamua niombe rufaa ya kwenda hospitali ya rufaa ya Bugando Mwanza na nikapewa na kwenda Bugando ambako nilikutana na dakitari bingwa wa kifua kikuu maana walifikiri ni ugonjwa wa kifua kikuu au ukimwi naye nilimpa picha za x ray nilizotoka nazo hapa Bukoba na akazikataa kwamba hawezi kuziamini hivyo wakanipiga picha nyingine za x-ray pale Bugando Mwanza na hata wao hawakuona tatizo lolote bali walinipa dawa nikarudi nyumbani. baada ya mwezi mmoja nikarudi tena Bugando na kupewa dawa nikarudi tena nyumbani. Na ikawa ni kawaida ya kwenda kila mara na kupewa dawa lakini bado nikawa siponi.

Siku moja katika safari yangu ya kwenda Bugando kwa ajili ya matibabu, nilipita sehemu moja inayoitwa miti mirefu karibu na Shule ya Sekondari ya Mwanza, kuna jengo moja la ghorofa ambalo halijaisha bado lakini mle ndani huwa kuna wapendwa walio okoka wanasalia mle ndani. na kila mara nilipokuwa nikipita pale hasa niwapo katika safari zangu za Mwanza nilikuwa nahisi kuvutiwa sana kwenda kuabudu nao na kuwasikiliza wanachohubiri. Lakini hata hivyo nilikuwa nasikia roho yangu ikisita sana. Wakati mmoja nikamuomba Mungu kwamba anipe nafasi ili siku moja nikienda Mwanza nipate nafasi ya kwenda siku za mwisho wa wiki na nipate nafasi ya kuabudia pale. Na kweli siku moja Mungu akanipa nafasi ya kwenda Mwanza siku za mwisho wa wiki hivyo Jumapili niliamka na kwenda asubuhi Bugando katika ibada iliyokuwa ikifanyika katika dhehebu langu na ibada ilipokwisha niliondoka kurudi nikipitia njia ile ile ya uchochoro wa kutokea miti mirefu na kufika katika kanisa lile nililokuwa nasikia kutaka kwenda kuabudia na kuona ni nini kinachofanyika ndani. Ndani ya jengo lile nilikuta ibada ikiendelea na mhubiri alisema leo lazima kuna muujiza utendeke sana hapa na hapo nilipata mshangao na kuhisi labda mhubiri ana nia na mimi. Na hapo nikasema ngoja nijiweke sawa na Mungu labda anataka kufanya uponyaji juu ya mwili wangu. Na ilikuwa kama saa 5 hivi maombi yalipoanza na yeye akasema kila mtu hapa lazima atanena kwa lugha mpya.

Mimi nilipata mshangao na kuona huyu bwana ni muongo kwani hata mimi naweza kunena kwa lugha?

Kweli Mungu ni mwema maana hata mimi sikuwa nimewahi kunena kwa lugha: lakini mhubiri aliomba sana na watu wengi walianguka chini na kuanza kunena kwa lugha lakini mimi sikuona mabadiliko. Katikati ya maombezi mhubiri alikatisha maombi na kusema naona kuna baadhi ya watu hawajaguswa na Roho mtakatifu. Hivyo akasema naona sasa inabidi tuanze maombi upya na ilikuwa kama saa 11 jioni. Kweli alianza kuomba upya na kweli Roho mtakatifu alishuka pale na niliona watu wengi zaidi ikiwa ni pamoja na mimi ambaye sikuwa nikiamini kuhusu kunena kwa lugha nikinena kwa lugha mpya.

Niliponena kwa lugha mara ilikuja roho ikipingana na jambo ili ndani ya moyo wangu. Nilifikiri nimechanganyikiwa na kitu kilichonipata si sahihi. Nilinyamaza na kutulia kimya. Nikapata wazo ebu nianze kuomba tena lakini kila nilipoomba nilijikuta narudia yale yale.

Hapo nilijua hiyo ilikuwa kazi ya Mungu maana hata nilipojaribu nibadilishe sikuweza.

Nilijitambulisha kama mgeni na kuwaeleza kuwa nimekuja Bugando kwa ajili ya matibabu na wao walinitia moyo kwamba hakuna haja ya kwenda Bugando tena bali nirudi kesho yake ili waniombee na niondoke kurudi Bukoba.

Niliingia mashaka kidogo kwa sababu nilikuwa na barua za kazi na zilihitaji kuwa na sahihi na mihuri ya dakitari. Ni kazini waliokuwa wamenipa fedha za matibabu na walihitaji kujua matokeo ya matibabu hivyo kama nisingefika hospitali ningepata matatizo kazini.

Siku iliyofuata nilipita pale kanisani nikawakwepa na kwenda hospitali Bugando ambako kwa kweli nilipata shida nyingi maana fedha iliniishia na dawa walizonipa kutumia kwa mwezi mmoja zilinisumbua kwa kunipa shida zingine, maana nilipata maumivu katika kila kiungo cha mwili na ilibidi niziache nisizitumie tena. Nilirudi tena Bugando na kuwajulisha kwamba dawa walizonipa zilinisumbua sana na wao wakanipa nyingine. Hata hivyo kuanzia siku hiyo nikamwambia Mungu kwamba ingawa sijapona mara hii ndiyo itakuwa siku yangu ya mwisho kuja Bugando maana hata wao hawezi kunisaidia. Nilimwambia Mungu kwamba nimeamua kukutumainia wewe tu.

Na siku si nyingi baada ya hayo yote kutokea nilikwenda kwenye msiba wa mtu mmoja na akawapo mhubiri aliyesema maneno fulani kutoka katika kitabu cha Zaburi 103: 3-4 "Akusamehe maovu yako yote, akuponya magonjwa yako yote, atakomboa uhai wako na kaburi." na hapo nikagundua kama kweli yeye ndiye aliyenisamehe dhambi zangu na huyo huyo ataniponya magonjwa yangu na kuniokoa na kaburi. Hivyo nilipata mahali pa kusimamia kukataa kurudi tena Bugando na sijarudi tena maana naona nimepona. Namshukuru Mungu upendo wake ni wa ajabu maana Sikujua kama nitaokoka kwani sikuwa na imani na wokovu. Lakini sasa nimeshaokoka.

Namshukuru Mungu pia kwa kunileta katikati ya nyie ndugu zangu wa fellowship hii maana mmekuwa ni msaada sana kwangu katika kunifundisha na kuniombea. Nilipokutana na mtumishi wa Mungu Kiongozi wa fellowship hii na kumuelezea matatizo yangu alikubali kuniombea maana nilikuwa pia na shida ya kupungua sukari ya mwilini.

Namshangaa Mungu kwani ninaweza hata kufunga kula chakula kwa muda wa siku saba kwa ajili ya maombi na nisipate shida yoyote. Zamani nisingeweza kukaa muda mrefu bila kula chakula chochote la sivyo sukari ingeweza kupungua na ningekosa nguvu na kuanguka. Mungu kaniponya na sasa najiona ni mwenye afya nzuri.

Nasikia kutiwa zaidi nguvu na neno la Mungu lililo katika 2Timotheo 2:19b "Kila alitajaye jina la Bwana na aache uovu"

 

 

RUDI UKURASA WA KWANZA

RUDI MWANZO WA UKURASA HUU