Ushuhuda wa Jimmy Kalugendo

BWANA YESU NDIYE CHANZO CHA BADILIKO KATIKA MAISHA YANGU

Bwana Yesu asifiwe sana kwa wema wake niliouona katika maisha yangu binafsi.

Nilimpokea Yesu Kristo mwaka 1996. Hii ni baada ya kuwa nimekwenda kuwatembelea ndugu zangu nyumbani kwao jioni moja. Pale nilikuta wakiwa na ibada ya nyumbani na kwa sababu sikuona haja ya kujitenga (ingawa ukweli sikuwa napenda) nilikubali kukaa na kusikiliza mtumishi akifundisha neno la Mungu.

Maneno mengi yalizungumzwa na nilisikia ndani ya moyo wangu kama yote yalikuwa yamenikusudia mimi maana nilikuwa kama vile mtu aliyevaa nguo lakini ghafla akavuliwa bila kupenda na kubaki uchi. Hivyo nilipata shauku ya kuwa ninakwenda kila jioni kusikiliza injili maana kila siku jioni, ibada ilikuwa ikifanyika pale nyumbani kwa ndugu zangu. Moyo wangu ulianza kuyeyuka na nilijiona kuwa hakika nahitaji kumpokea Yesu na awe Bwana na mwokozi wangu kwani nilisikia mengi na shuhuda nyingi za matendo ya ajabu aliyofanyia watu wengine.

Hata hivyo haikuwa rahisi maana hata kabla ya hapo wahubiri wengi walikwisha nihubiri lakini siku zote nilikuwa mbishi na nilidhani haya ni mambo ya kidhehebu na kidini tu. Kamwe sikuamini kwamba mtu unaweza kubadilishwa na Bwana Yesu na kuwa kiumbe kipya. Niliona waliookoka kama watu walio changanyikiwa na kupoteza mwelekeo wa maisha. Maisha yangu hayakuwa mazuri hata kidogo maana nilitawaliwa na dhambi za kila aina. Sikuwa mlevi wa pombe wala Sigara kama wengine, maana hayo yote nilikuwa nimeyaacha miaka ya '80 lakini nilitawaliwa na dhambi zingine nyingi ikiwamo na uzinifu. Sikuwa na furaha wala amani maana hata familia yangu ilikosa upendo na kuwa katika hali ya magawanyiko. Nilihisi kukataliwa na kuonekana asiyefaa katika familia yangu. Nilijawa chuki, hasira, hali ya kulipiza kisasi, kutokuwa muaminifu, na ukatili wa kila aina. Hali hii ilinisukuma zaidi kuendelea kuishi katika maisha ya dhambi. Amani ilitoweka kabisa na nikabaki kama mtu aliye katika kisiwa tu. Sikujua wala kuamini kuwa ninaweza kupata msaada na hata nilipoambiwa kwamba upo msaada sikukubali. Nilibaki nikitumia akili zangu na kuangalia kwa macho yangu na nikabaki nikijihukumu mwenyewe.

Mimi ni mfanya biashara na nilikuwa na fedha nyingi tu na pesa kwangu halikuwa tatizo. Nilikuwa na gari 3 na nyumba ndogo ya kuishi. Sikuwa na tatizo la kifedha kama wengi walivyokuwa lakini bado amani ilikuwa haba kwangu. Fedha haikuleta suluhisho.

Pole pole nilianza kufuatilia maandiko niliyokuwa nikisikia mtumishi akifundisha kule kwa ndugu zangu kwa kuisoma biblia niliyokuwa nimepewa zawadi ( ingawa siku zote sikuwa naisoma bali ilikuwa katika shelf tu ili nami nionekane ni mkristo!) miaka kadhaa kabla. Kule kuanza kuisoma tu kulinipa changamoto na kunifanya nianze kuisoma kwa bidii zaidi. Niliona jinsi Mungu anavyochukia dhambi lakini pia alivyojaa huruma kwa wote wanaotubu na kujitenga nayo. Nilisukumwa zaidi kuanza kusoma vitabu vya agano la kale kuanzia kitabu cha Waamuzi, Samweli, Wafalme, Nyakati na Isaya. Hakika kama Mungu anakusudi nawe, naamini huna jinsi ya kumkimbia kwani kila niliposoma maneno ya Mungu katika vitabu hivi nilikuwa naona kama kuna mtu anaye ninyooshea kidole kuniambia kuwa hapa Mungu anakusema wewe. Na hili liliniongezea shauku ya kutaka kujua nini Mungu anakusudia katika maisha yangu. Na kusema kweli ilifika wakati nilikuwa naacha hata kwenda kazini na kukaa ndani siku mbili nikisoma maandiko kutafuta ukweli. Nilibaki nikimuomba Mungu na kulia sana mara kwa mara na hasa kila nilipokuwa kitandani nyakati za usiku na nilipokuwa nikiitafakari nafasi yangu katika ufalme wa Mungu maana niligundua mimi niko mbali naye, Isaya 57:21 inasema wazi kuwa hakuna amani kwa wabaya.

Niligundua ni dhambi tu iliyokuwa ikinitenga na uso wa Mungu na kunikosesha amani. Huko kazini na mitaani rafiki zangu hawakujua shida iliyokuwa moyoni mwangu. Wengi waliniona kama mtu mwenye mafanikio na asiye na shida yoyote lakini kwa vile si rahisi mtu kutambua mawazo ya moyo, wasingeweza kufahamu jambo hili. Niliona neno la Mungu likiwa linanionyesha wazi kuwa kila aliyetubu dhambi na kuiacha huyo Mungu alimrudia. Nayo 2 Nyakati 7:14 iliendelea kuniongezea nguvu hivyo kwamba nikaona ni vema nijiachie kwa Bwana Yesu ambaye niliona kitabu cha Isaya 7:14 na 53:1-12 kikisema habari zake. Niliamua kumpa YESU maisha yangu.

Kwa sababu ya hali ya kuwa katika dhambi nilikuwa na kipindi cha kadri ya miaka 5 nikiwa siudhurii kanisani na kwa mara ya kwanza nilianza hata kwenda kuabudu nikisikia uhuru kabisa. Nilianza kusikia kutamani kukaa katika neno la Mungu na kulitafakali kila wakati na hapa nilianza maisha mapya ndani ya Yesu. Baada ya miezi kama minne nikiwa nimekwisha okoka, siku moja usiku niliamka na sikupata usingizi kabisa. kwa kuwa nilisha anza kujifunza kuomba katika ibada nyumbani kwa ndugu zangu niliamka na kuanza kuomba na kwa kweli niliomba kwa muda mrefu kidogo. Baada ya maombi marefu nilisikia kama sakafu ya pale kitanda changu kilipokuwa ikipasuka kwa kishindo kikubwa. Na kwa kweli nilisitisha maombi na kukaa kimya kwa uoga huku nikitafakari ni yapi yaliyotokea. Katika kipindi hiki nilikuwa peke yangu chumbani. Baada ya kutafakari na kuwaza sana! mambo mengi yalianza kupita katika mawazo yangu, na mara ghafla nilisikia sauti ya mtu ikisema na mimi ana kwa ana kuwa "JE MAMBO UNAYOPANGA KUFANYA KESHO UNAONA NI YA MAANA KULIKO KWENDA FELLOWSHIP?". Huo ulikuwa ni usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili. Sikuwa nimewahi kwenda fellowship wala sikuwa nimepanga kwenda huko. Sikujua iliko fellowship wala halikuwa katika mipango yangu. Niliamka na kuwasha taa chumbani lakini sikumuona yeyote aliye zungumza nami; na hii iliniongezea wasiwasi maana kwa kuanzia ilikuwa inasitisha hata baadhi ya mipango niliyokuwa nayo tayari kwa ajili ya Jumapili. Nilizoea kutembelea marafiki kupiga soga tu kila jumapili jioni maana sikuwa na la kufanya zaidi ya hapo.

Jumapili asubuhi baada ya ibada kanisani, niliamua kumfuata mdogo wangu ambaye tayari alikwisha kuokoka siku nyingi na nilikuwa na kawaida ya kumuuliza kila swali la mambo yote yaliyonitatiza au kuwa mageni katika maisha yangu mapya ya wokovu. Nilimuelezea kuhusu sauti ya ajabu niliyoisikia na yale iliyoniambia. Na ni yeye ambaye aliniambia kuwa hiyo ilikuwa ni sauti ya Yesu na anajua ninapotakiwa kwenda. Hivyo jioni ya siku hiyo alinichukua na kunipeleka Tumaini Shule ya Msingi kwenye fellowship. Na hapo ndipo safari yangu ya baraka na kumtumikia Mungu ilipoanzia.

Tangu siku ya kwanza nilipokwenda katika fellowship nilijisikia kama nimefika katika sehemu yenye baraka na msaada kwani Yesu aliendelea kukutana na mimi pale, huku akiwatumia watumishi wake mbalimbali kunihudumia na kuhakikisha nasonga mbele katika maisha yangu ya kiroho. Nimepata msaada wa kulelewa na sasa hata mimi nimeshazaa matunda ambayo nayo yanaendelea kukua. Na si hilo tu bali nimekuwa baraka kwa kanisa la Bwana Yesu mwenyewe.

esu ni mwema na wa ajabu na tena kajaa upendo na huruma. Anachojali yeye ni kuona kuwa je wataka msaada?, je wataka kusamehewa?, je wataka amani? Na hapo yeye huwa tayari kukupa. Unachotakiwa ni kumwambia NDIYO nataka. Hata rafiki zangu hawakuwahi kuamini kuwa nimeokoka maana walinijua na kufahamu maisha yangu maovu ya zamani. Walidhani haitakuwa rahisi kubadilika (mawazo ambayo hata mimi niliwahi kuwa nayo!) lakini hawakujua kuwa mabadiliko yote chanzo chake ni Bwana Yesu mwenyewe. Leo hii wote wamekubali kuwa yamkini Yesu anaweza kubadilisha maisha ya mtu, kama alivyobadilisha maisha yangu. Rafiki zangu wengi niliokuwa na ushirika nao wameshakufa kwa ukimwi lakini mimi Yesu aliniacha niwe huru na niwe ushuhuda kwa mataifa kuwa Yesu ndiye chimbuko la mabadiliko yetu. Yeye ni Bwana wa wokovu wetu. Jina la Bwana liinuliwe na kutukuzwa milele na milele. Bwana Yesu apewe sifa na kila kiumbe kwa kujitoa kwake kuwa sadaka kwa ajili yangu.

Amen, Amen, na Amen.

 

 

RUDI UKURASA WA KWANZA

RUDI MWANZO WA UKURASA HUU