USHUHUDA WA WANAFUNZI WALIOOKOKA

BUKOBA SEKONDARI 2000-2001

Na ashukuriwe Bwana Mungu wetu ambaye ujidhihirisha katika maisha ya wateule wake. Kama ilivyoandikwa katika Mithali 8:17, tuligundua kuwa pindi umwitao Bwana naye hujifunua na kukuonyesha mambo makubwa .Hivyo basi ufuatao ni ushuhuda wa wanafunzi waliomtumainia Bwana kuweza kushinda mitihani yao vizuri:-

Kwanza ni suala la uinjilisti. Kutokana na kwamba wanafunzi waliookoka walijitoa sana kwa habari ya kuhubiri injili Mungu alijidhihirisha kupitia wanafunzi, uimbaji ukaimarika hivyo basi Mungu akawa anasifiwa katika Roho na kweli. vile vile upako wa kushuhudia ulizidi kuongezeka hadi shule nzima nazo shule nyingine wakajua kuwa wapo waliookoka shuleni hapa.

Katika hali ya kushamiri kwa injili shuleni naye shetani alijiinua kupitia utawala wa shule lakini tunamshukuru Mungu kwani tulisimama imara. Na hata ilitokea kusimamishwa mbele za wanafunzi wote na tukatishiwa kufukuzwa shule eti tunabadilisha dini za watu. Tulilofanya ni kuomba na baadaye tulipelekwa katika ofisi ya mkuu wa shule, na kwa ufupi ni kwamba hilo halikututisha kwani Roho mtakatifu alitupatia majibu na kesi haikuendelea nasi tukaendelea kuhubiri injili.

Kuhusu maombi. Ilikuwa ni utaratibu kwamba kila ijumaa ni siku ya maombi ya kufunga. Wakati wa kifungua kinywa "breakfast" ndio ulikuwa muda mzuri wa kuyazungukia madarasa na kuombea wanafunzi, na matokeo yake ni kwamba wanafunzi walizidi kuwa na kiu ya neno la Mungu. Wakati wa mikutano ya UKWATA wanafunzi walihudhuria kwa wingi kutoka madhehebu mbalimbali na pia ni wakati tulioutumia kuhubiri injili.

Vile vile kwa upande huo huo wa maombi karama ya uponyaji ilionekana ikitenda kazi kwani wanafunzi wengi hata ambao hawajaokoka waliamini kuwa Yesu ni mponyaji kwani tulisimamia neno la 'kwa kupigwa kwake sisi tumeponywa" hivyo basi magonjwa na roho chafu zilifutiliwa mbali kwa jina la Bwana Yesu.

Kwa kuongezea ni kwamba tulifanikiwa kuhubiri injili kwa wanafunzi na walimu kupitia vipeperushi "tracks" za "SALAMA KONDOO". Hizi zilikuwa msaada kwa jumuhiya nzima ya shule, kwa hiyo basi maswali tulipata mengi na ndio ulikuwa muda mzuri wa kuwahubiri injili na kuwaongoza sala ya toba.

Baada ya mlipuko wa wokovu kuongezeka ilitubidi tuanzishe "FELLOWSHIP" lakini kwa muda mfupi utawala wa shule uliisitisha. Kwa kuwa Mungu ni mkuu tuliongozwa kumshirikisha mchungaji Elisha Bililiza suala hilo ndipo alipotukaribisha katika kanisa la Anglican. Kila ijumaa tukawa tunakutana na kumegeana vipawa kwa kadri tulivyojaliwa na roho mtakatifu. Vile vile Mungu ametutumia hata sehemu mbalimbali kwa kuhubiri injili kwa njia ya nyimbo na hata ushuhuda. Baadhi ya wenzetu walijaliwa kupata nafasi za kwenda nchi za nje ili kumshuhudia Bwana Yesu mfano ni:- Nancy Rwezimula aliyefanikiwa kwenda Sweden kwenye mkutano wa kiroho wa vijana ulimwenguni. Kundi lingine lilikwenda Ujerumani kuhubiri injili kwa njia ya nyimbo ambao baadhi yao ni Evancy rutabingwa, Francis Lutalala, Nancy Rwezimula na wengine. Hivyo basi kwa kupitia sisi ushuhuda ulienea hata huko mbali. Vivyo hivyo kwa habari ya masomo Mungu alijifunua na kutupigania. Katika masomo yetu tulisimamia Kumbu kumbu 28:13, ndipo tulipata na pambio la " mimi ni kama Mungu alivyosema mimi wa kwanza siyo wa mwisho" hivyo basi taaluma yetu pia ilikuwa juu kulinganisha na wanafunzi wengine darasani.

Katika hali ya kimwili masomo yalikuwa magumu ila Mungu alitushindia, mfano kwa wanafunzi waliomaliza 2001 wakiwa ndani ya Yesu ambao ni Evancy Rutabingwa, Daniel Nkungu, Francis Lutalala, Menchidia Rwabunywenge, Alice Julius, Angelina Michael, Danstun Raphael, Jenerose Jonathan, Anitha Lugambwa na wengineo Mungu amewashindia mitihani yao na sasa wanaendelea katika vyuo mbalimbali vya elimu ya juu Tanzania.

Kwa kuongezea tulikuwa tukiomba kwa ajili yetu sisi pia na darasa zima hivyo basi darasa zima lilikuwa na uelewa wa hali ya juu hata kubadilisha historia ya shule kitaaluma. Hii ilitokana na maombi kwani si kwamba wanafunzi walikuwa na akili nyingi.

Hata hivyo Mungu anazidi kujidhihirisha kupitia watakatifu wake waliobaki pale shuleni na kazi ya Bwana inazidi kusonga mbele. Mungu aibariki kazi ya mikono yake sasa na hata milele.

 

 

RUDI UKURASA WA KWANZA

RUDI MWANZO WA UKURASA HUU