MTU ALIYEOKOKA NI WA THAMANI MBELE ZA MUNGU.

Mtu aliyeokoka anahesabiwa kama mtu wa thamani sana mbele za Mungu. Nini maana ya uthamani mbele uso wa Mungu? Maana ya uthamani huo ni kuwa mtu aliyeokoka yuko katika mpango maalumu wa Mungu. Ina maana kuwa mtu aliyepata neema ya wokovu si kwa ajali au kwa bahati mbaya bali ni kwa mpango maalumu wa Mungu mwenyewe. Mungu katika uumbaji wake alikua na mpango maalum.Alituumba kwa ajili ya utukufu wake sisi tulioitwa kwa jina lake. Mungu ameruhusu uzaliwe katika familia uliyomo kwa makusudi kabisa. Kwa sababu yeye alituumba kwa ajili ya makusudi yake mwenyewe. Isaya 43:7

Isaya 43:4 Kwa kututhamini hivyo Mungu tayari ametujengea mazingira fulani ya ulinzi wake kama yalivyo mapenzi yake.

Yeremia 1:4-7 Ili kudhihirisha kuwa ni wa thamani mbele zake bado Mungu anatudhibitisha kuwa alitujua hata kabla ya kuumbwa na tukafanyika watu, pia alitutakasa kabla ya kuzaliwa. Mungu alimwambia Yeremia kwamba alimjua kabla hajamuumba. Mungu alimuandaa Yeremia mtoto mdogo kwa kazi maalumu, ya kubomoa, kuharibu na kuangamiza kisha kujenga na kupanda. Bwana anahitaji kututumia kwa ajiri ya kazi yake, kama aliweza kumtumia Yeremia katika umri mdogo aliokuwa nao kwa kukosa ila kutumia bali ni mpango wake yeye mwenyewe kumtumia yeyote katika umri wowote ule. Hivyo nasi basi tumeokolewa kwa ajili ya kazi maalumu ya Mungu mwenyewe si kwamba anakosa wa kuokoa au kuomba anahitaji sana na watu wa kufanya nao. Mungu anampango maalum juu ya maisha yetu hatuko katika kizazi hiki kwa bahati mbaya. Hata kama hauna kisomo usijali wala kujilaumu bali mtafute Mungu ili ujue kusudi lake kwake ni nini .Mungu amekuweka mahali ulipo ili uwe kisababisho cha yeye kuinuliwa mahali hapo ulipo. Sisi ni watu maalum na Mungu anataka kujidhihirisha kwa wanadamu kupitia sisi. Watu wa Mungu wengi tunashindwa vita vya kiroho kwa sababu ya kujiangalia jinsi tulivyo lakini tunapaswa kujua kwamba Mungu anatupenda na anatuthamini sana Tujue kwamba sisi ni wa thamani mbele za Mungu. Shetani mara zote anapotaka kutushambulia kwanza anatuma wajumbe wake kupeleleza watu wa Mungu wakoje kama tuko imara au legelege. Tatizo Kubwa linalokuja kujitokeza kwa watu wa Mungu ni kujidharau, kujiona hatuwezi wala hatufai. Na huo si mpango wa Mungu kwamba tujione hatufai bali Mungu anapotuokoa tayari anakuwa na mpango maalumu juu ya maisha yetu na anahitaji tufanye kazi yake jinsi anavyotuamuru. Tusijidharau Mungu ana makusudi makubwa na siri na nguvu tutakazo tumia sio zetu ni Mungu mwenyewe .

Zaburi 136. Muimbaji wa Zaburi akimuomba Mungu alimuona kama wa ajabu mno kwa mambo makuu anayoyafanya usiku na mchana.

Zakaria 4: 6; Yeremia 1:9-10; 2Nyakati 16: 9. Macho ya Mungu yanazunguka ulimwenguni kote kutazama wale walio wakamilifu wa moyo kuelekea kwake ili ajionyeshe kuwa yeye ni mwenye nguvu . Mungu anatuandaa katika katika huduma kwa hiyo anatuangalia uaminifu tulionao katika vichache tulivyo navyo Tukumbuke Mungu alikotutoa ili tuweze kumtumikia Mungu hadanganyi kwani yeye ni mkweli na uaminifu wake ni kizazi hadi kizazi. Je kama Bwana asingejidhihirisha katika kanisa la kwanza, sisi msingi tungepata wapi? Hatuwezi kubeba utukufu huku ukiwa na kiburi pamoja na majivuno. Kumbuka Mungu ametuumba kwa makusudi ili atutengeneze, na tumeitwa kubomoa na kuangamiza ili tujenge kwa hiyo tuwe watii ili tulifanye imara agano lake Mungu ana makusudi maalum kwa kila kinachotokea katika maisha yako kwa sababu sisi ni vyombo vya Mungu thamani

Mungu anahitaji sana kututumia na ndio maana macho yake yanatazama duniani yanakimbia kimbia huko na huko ili apate kujionyesha kuwa ana nguvu juu ya wenye moyo wa kumuelekea yeye.

Tunachohitaji kufanya na cha kutusaidia ili tuzidi au tuweze kuwa wa thamani mbele za Mungu ni kuzidi kutafuta yaliyo mapenzi yake ili hatimaye tujikute tuko ndani ya lengo la Mungu mwenyewe alilotuitia na si nje ya mpango wa Mungu. Mungu ametuokoa kwa kusudi maalumu na Mungu akubariki.

Mafundisho haya yametolewa na Mchungaji Benard Benedicto.

 

 

RUDI UKURASA WA KWANZA

RUDI MWANZO WA UKURASA HUU