KIWANGO CHA MUNGU - DOUBLE AGENT

KUTUNZA KIWANGO CHA MUNGU KATIKA KIZAZI CHETU

(DOUBLE AGENT)

UTANGULIZI.

Pamoja na mabadiliko makubwa ya nyakati zetu katika siasa, uchumi utamaduni (maadili) na kidini. Mungu anacho kiwango chake ambacho ndicho anakubaliana nacho katika maisha yetu. Ili tuweze kuishi na kufiti katika mipango na makusudi yake ni lazima tuangalie kukitunza kiwango cha Mungu katika maisha yetu.

“Kwa kuwa mimi Bwana si kigeugeu (sibadiliki)” Malaki 3:6 Biblia inaonyesha kuwa tumeitwa na tumfananie Mungu na kamwe si Mungu atufananie sisi. Kwa hali hiyo kama hali yetu haifanani na Mungu wito ni sisi kubadilika na wala si Mungu abadilike awe kama tunavyotaka sisi au rafiki zetu, mazingira yetu au jamii. Biblia huonyesha kuwa sisi tunabadilishwa toka UTUKUFU hadi UTUKUFU. Mungu anatunza kiwango chake na kiwango cha Mungu kinakwenda sawa sawa na Neno lake.

Biblia huonyesha mtu hufanana na mawazo yake. “Maana aonavyo nafsini mwake, ndivyo alivyo…”.Mithali 23:7 (Tafsiri ya King James hutumia kufikiri badala ya kuona katika nafsi.) Neno la Mungu ni mawazo ya Mungu; kwa hiyo linamfunua Mungu vile alivyo. Ili tumfananie Mungu inabidi tulitafakari Neno lake. Ndipo litaumba picha ya ki-Mungu katika mawazo yetu. Wala tusifanye kuifuatisha dunia na kuwaza ya dunia tu.“Wakuu wa Yuda ni kama watu waondoao alama ya mpaka; nitawamwagia ghadhabu yangu kama maji” Hosea 5:10

Wito wetu ni kutunza kiwango cha Mungu. Sisi ni vielelezo. Kiwango cha Mungu kinamtambulisha Mungu wetu katika jamii kama Jehova Nissi. Yaani yeye ni bendera yetu. Mfano mzuri ni jinsi Musa katika vita dhidi ya Amaleki alivyonyanyua kiwango cha Mungu (fimbo iliyowakilisha mamlaka ya Mungu) na hapo Joshua alishinda vita. Watumishi na viongozi wa kiroho wakinyanyua kiwango hiki ambacho ni neno la Mungu kina Joshua (kanisa) wanashinda vita. Kiwango kikiondolewa kanisa na taifa hupoteza mwelekeo. Kutoka 17: 11-15

DOUBLE AGENT

Kuna watu ambao katika ujasusi( upelelezi) hufanya kazi pande zote mbili huku kila upande ukiamini unafanyiwa kazi wenyewe. Double agent anakubalika pande zote na hulipwa mshahara na pande zote. Na katika ujasusi huyu ndiye mtu wa hatari ambaye akipatikana hawezi kusamehewa. Ndani ya kanisa pia wamo double agents. Kanisa la Laodikia walionywa kuacha tabia hii mbaya.

“Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala moto (wewe ni double agent);” Ufunuo 3:15 Haiwezekani kutunza kiwango cha Mungu kisha ukaonekana kote kote. Lazima uweke msimamo na dira itakayotambulisha matakwa na kiwango cha Mungu.

Ni lazima tufike mahali tunamtambulisha Mungu katika kila hatua ya maisha yetu kwa viwango vyaUPENDOwetu,UAMINIFU, USAFI, UVUMILIVU, UKARIMU, HURUMA, UNYENYEKEVU NA UTII.Sharti ifikie hatua maisha yetu yanaakisi hali ya Mungu wetu. Hapo tunaweza kuwa manabii( wasemaji wa Mungu) kwa kizazi chetu. Watu wanaotuona wapate ujumbe wa jinsi Mungu alivyo na anavyotaka katika maisha yao. Hatuwezi kuridhia maovu na kuchukuliana na udhaifu wa dunia hii na bado tutegemee kuwa nuru. Mungu atusaidie kuwa watu wanaosimamia kiwango cha Mungu katika siku zetu na hapo maisha yetu yatakuwa na faida katika ufalme wa Mungu.

Mungu akubariki.

 

 

 

RUDI UKURASA WA KWANZA

RUDI MWANZO WA UKURASA HUU