MASOMO YA UFALME WA MUNGU

HATUA YA KWANZA

KUUINGIA UFALME WA MUNGU

Leo hii tungemwuliza Mungu ni jambo gani lililo muhimu sana katika moyo wake analohusika na kufuatilia kwa karibu zaidi hapa duniani angesemaje? Tunaweza kuwa na majibu mengine lakini naamini UFALME WA MUNGU ndio agenda ya kwanza kabisa katika moyo wa Mungu.

Hata baada ya Yohana kutiwa gerezani, Yesu akaenda Galilaya akihubiri Habari Njema ya Mungu. akisema Wakati umetimia, na UFALME WA MUNGU umekaribia tubuni na kuiamini Injili. Marko 1 :14

Hayo ndiyo mahubiri ya kwanza Bwana Yesu aliyofanya; akatambulisha kuwa huduma yake duniani inatambulisha ujio wa UFALME wa Mungu duniani. Kwa Nikodemu akasema ili kuuona UFALME wa Mungu lazima kuzaliwa mara ya pili.

“ mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho hawezi kuuingia ufalme wa Mungu.” Yohana 3:5

Hapa tena Bwana Yesu anasema kuna KUUONA lakini kusudi la Mungu ni KUINGIA. Sharti la kuingia ni KUZALIWA KWA MAJI na KWA ROHO. Hapa tena si maji ya mtoni, tunajua biblia inajifafanua yenyewe na kamwe haijipingi. Kuhusu kuzaliwa mara ya pili sehemu zingine anasema hivi:-

“Kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu iharibikayo bali kwa ile isiyoharibika: kwa neno la Mungu lenye uzima lidumulo hata milele.” 1 Petro 1:23 Je kuna uhusiano gani kati ya Neno na Maji? Linganisha na Efeso 5:25 “ Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili makusudi alitakase kwa maji katika neno…" Hivyo katika kuzaliwa mara ya pili Neno la Mungu huleta uzima wa milele ndani ya roho ya mtu anayeliamini na hapo roho ya mtu uhuishwa na kuzaliwa upya kwa uwezo wa Roho Mtakatifu!

“lakini wema wake Mwokozi wetu Mungu na upendo wake kwa wanadamu, ulipofunuliwa, alituokoa; si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyotenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu". Tito 3:4-5

Watu wanaposikia Habari Njema ikihubiriwa wakaiamini ile Injili nguvu ya Mungu katika neno lake huuleta ufalme wa Mungu katika moyo wa mtu. Na hapo UFALME wa Mungu hupanuka kwa kuwa na kituo hapa duniani ambako matakwa ya mfalme yanatekelezwa. Ndani ya moyo wa mwamini. ‘ …ufalme wa, Mungu hauji kwa kuuchunguza; wala hawatasema, Tazama, upo huku, au, kule, kwa maana, tazama, UFALME wa Mungu umo ndani yenu". Luka 17:20-21. Hii ni serikali ya Mungu, mamlaka na nguvu ya Mungu katika moyo wa mwanadamu. Hapo Mungu anatekeleza malengo yake kupitia mtu aliyekubali kumtii apitishe mawazo yake kwake; nguvu za Mungu zinatimiza matakwa ya Mungu kupitia duniani. Duniani anayeonekana ni mwanadamu lakini kinachofanyika ni cha Mungu. Mtu anakuwa ni station ya siri inayofanya mambo ya UFALME wa Mungu ndani ya falme za dunia hii. Ukipenda kuwa sehemu ya mpango huu wa ajabu lazima kutubu na kuiamini Injili.

Ikiwa hii ni shauku ya moyo wako basi Sali sala hii ukimaanisha toka moyoni mwako.

Mpendwa Bwana Yesu nakushukuru kuwa umeleta ufalme wa Mungu hapa duniani. Nakubali kuwa nimeishi nje ya matakwa ya Mungu na hivyo kumhuzunisha Mungu. Naomba unisamehe dhambi zangu zote. Naufungua moyo wangu nikikuribisha ndani ya maisha yangu. Kuanzia leo naomba unitawale. Nitakutii na kukufata siku zote zilizobaki za maisha yangu. Ahsante kwa kuniokoa katika jina la Yesu ninaomba Amen.

 

 

RUDI UKURASA WA KWANZA

RUDI MWANZO WA UKURASA HUU