MASOMO YA UFALME WA MUNGU

UFALME UNAPOTOLEWA NA PIA KUONDOLEWA

Utangulizi

“sikilizeni mfano mwingine. Kulikuwa na mwenye nyumba, naye alipanda shamba la mizabibu, akalizungusha na ugo, akachimba shimo la shinikizo ndani yake, akajenga mnara, akapangisha wakulima, akasafiri. Wakati wa matunda ulipo kuwa karibu , akawatuma watumwa wake kwa wale wakulima, wapokee matunda yake. Wale wakulima wakawakamata watumwa wake, huyu wakampiga, na huyu wakamwua , na huyu wakampiga kwa mawe….mwishowe akamtuma mwanawe kwao, akisema Watamstahi mwanangu. Lakini wale wakulima …..wakasemezana ….haya na tumwue, tuutwae urithi wake,…Basi atakapokuja Bwana yule Bwana shamba la mizabibu atawatendaje wale wakulima?

Katika habari hii tunamwona Bwana Yesu akitoa mfano juu ya ufalme wa Mungu. Jambo muhimu ni kuona huyu mwenye shamba aliwekeza katika ukulima. Ilimgharimu kujenga nyumba, kulima shamba na kujenga shinikizo. Biblia inasema aliwapangisha watu. Hivyo kulikuwa na makubaliano. Hitaji au faida ya mwenye shamba ni mavuno au matunda. Jambo la kushangaza wakulima hawa hawakutaka kumpa mwenye shamba kitu chochote badala yake waliamua kuwa wakali na wakatili.Wamejaa mawazo ya kujinufaisha wao wenyewe.

HATARI YA KANISA LA SIKU ZETU NI UBINAFSI

Tunaishi katika siku ambazo ubinafsi umefikia hatua mbaya. Watu wanataka kujinufaisha wao wenyewe na mazao ya mwenye shamba ambaye ndiye Bwana wa Mavuno. Lakini na ijulikane leo YUPO MWENYE SHAMBA. Ikiwa umepewa watu wengi au wachache, watu wazima au watoto lakini ujue YUPO MWENYE SHAMBA. Watumishi wa Mungu tumewekwa kuwa waangalizi na watunzaji wa hilo shamba. Punde mwenye shamba atarejea maana ni wakati wa mavuno.

MATUNDA YA UFALME NI NINI?

Matunda yanatajwa hapa yanamaanisha matokeo ya jitihada fulani. Katika ufalme wa Mungu jitihada zetu Mungu anategemea zitoe matokeo fulani.

Maana ufalme wa Mungu si kula wala kunywa, bali ni haki na amani na furaha katika Roho Mtakatifu. Warumi 14:22

Haki

Mungu anategemea huduma za watu wa Mungu zitoe haki. Haki inamaanisha ile hali ya kuondolewa hatia katika maisha ya watu. Haki hii ni ile inawafanya watu wastahili mbele za Mungu. Unapokuwa na haki una ujasiri. Mungu anapenda watu wanaokuja kwa ujasiri mbele yake huku wakijua kuwa anawakubali na anawapenda. Lakini tatizo ni hukumu mbaya iliyomo katika mioyo yetu juu ya dhambi zetu. Kamwe hali hii haiwezi kumpa mtu ujasiri mbele za Mungu badala yake inajenga woga na wasiwasi unaosababisha watu kuukimbia uso wa Mungu.

“Wapenzi miyo yetu isipotuhukumu, tuna ujasiri mbele za Mungu; na lolote tuombalo twalipokea….1 Yohana 3:21

Tatizo kubwa katika maisha ya watu ni dhambi ndiyo inayonyonya ujasiri wote mbele za Mungu. Neno la Mungu husema Ndiyo maana Yesu alikuja ili atuchukulie hatia yetu na kwa damu ya thamani afanye upatanisho kwa damu yake. Hivyo damu ya Yesu inafuta uovu na kutufanya wenye haki. Ni lazima watu wafunzwe kile ambacho Yesu amefanya kwa ajili yao katika kifo cha msalabani ili waweze kupokea ukombozi na msamaha wa dhambi. Ili huduma zetu zimzalie Bwana matunda lazima tueneze ukweli huu.

“ basi si zaidi damu yake Kristo, ambaye kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na mawaa, itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu mpate kumwabudu Mungu aliye hai? Waebrania 9:14

Amani

Ndiyo ile hali ya utulivu na ushwari unaokuja katika maisha kwa sababu tumeweka maisha yetu mikonnoni mwake. Amani huja kwa sababu yule tunayemwamini ni mwaminifu. Katika dunia hii iliyojaa wasiwasi na hofu na mashaka amani ya Mungu katika maisha yetu hutufanya kuwa watu tofauti. Hata katikati ya dhoruba bado tunajua

"Nasi twajua mambo yote hufanya kazi pamoja kwa ajili ya kutokeza mema kwa wale wanaompenda Mungu; wale waliotwa kwa kusudi lake”Warumi 8:28 (Kutoka Biblia ya King James Version)

Furaha.

Hii nayo ni hali ya kuburudishwa katika maisha yetu kutoka kwa Mungu mwenyewe. Tunajua kuwa kila mwanadamu analo hitaji la kufurahi. Lakini watu wengi hutafuta furaha nje ya Mungu katika tamaa zao. Kwa bahati mbaya furaha hizi zinadumu kwa kitambo tu majaribu yakitokea, furaha hizo hutoweka kama moshi. Lakini iko furaha isiyotegemea chanzo cha kidunia. Furaha ambayo inatokana na uwepo wa Mungu. Tukiwafundisha watu wa Mungu jinsi ya kuja katika uwepo wa Mungu katika ibada halisi katika Roho mara huzuni zao zitatoweka na watajazwa na furaha.

“Utanijulisha njia ya uzima; Mbele za uso wako ziko furaha tele; Na katika mkono wako wa kuume Mna mema ya milele". Zaburi 16:11

Na ikiwa sisi kama wapangaji wa shamba tunamletea Bwana wa mavuno matunda haya katika huduma zetu na katika watu aliotuamini kuwaangalia hapo tu ataridhika nasi. La sivyo kuna ukweli wa kutisha.

UFALME UNAPOONDOLEWA.

“ Kwa sababu hiyo nawaambia ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu, nao watapewa taifa jingine lenye kuzaa matunda yake.” Mathayo 21:43

Hivyo ndivyo Yesu alivyohitimisha mfano huu wa wapangaji na mwenye shamba. Kumbe ufalme unaondolewa na kutolewa. Mungu atusaidie sana tutaendelea tu kuwa na ufalme muda ule tunaouzalia matunda. (Tena angalia si kila tunda lolote linaloletwa kwa Bwana kama wengi leo wanavyojaribu kuleta mbele za Bwana. Ni yale tu matunda ya ufalme.) Katika historia ya kanisa tunaona katika nyakati mbali mbali ufalme ukitolewa na kuondolewa. Ukiondolewa mara nyingi walionyanganywa huwa hawajui umeisha ondoka. Wao hubaki na taratibu na zile kawaida lakini kile kitu halisi hakipo tena. Utaona kuna mfano tu wa utauwa lakini hakuna nguvu za kuishi hayo maisha ya utauwa tena. Linabaki jina la kuwa hai lakini watu wamekufa! Huu ni ukweli wa kutisha.

Ikiwa huduma, au kanisa la mahali fulani au movement yoyote nzima, na haizalishi matunda ya haki, amani na furaha katika Roho Mtakatifu katika wale inaowahudumia basi jua hakika ufalme walishanyang'anywa. Wanaweza kuwa na historia ya kuvutia jinsi Mungu alivyojidhirisha na kutenda zamani kati kati yao lakini hiyo haimaanishi bado yupo tena kati kati yao..

Mungu atusaidie tuzae na tutunze matunda ya ufalme.

 

 

RUDI UKURASA WA KWANZA

RUDI MWANZO WA UKURASA HUU