KUSHINDANIA IMANI.

Historia imejaa simulizi ya watu waliotetea na kushindania imani zao dhidi ya upinzani.

Wapenzi nilipokuwa nikifanya bidii sana kuwaandikia habari za wokovu ambao ni wetu sisi sote, Naliona imenilazimu kuwaandikia, ili mwonyane kwamba mwishindanie imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu. Kwa maana kuna watu waliojiingiza kwa siri, watu waliondikiwa tangu zamani hukumu hii, makafiri, wabadilio neema ya Mungu wetu kuwa ufisadi, nao humkana yeye aliye peke yake Mola, na Bwana wetu Yesu Kristo. Yuda 1:3

Yuda anawatia moyo watu wa Mungu kusimama kidete dhidi ya ukengeufu wa nyakati zake na kuitetea imani ya kweli. Watu wenye hila waliingiza mafundisho ya uongo katika kanisa ili kupotosha imani. Inashangaza leo jinsi watu wengi wanavyojitoa kufuata na kutetea imani kengeufu na mafundisho mapotofu kuishi. Haki za mashoga, imani za waganga wa kieneyeji, kujitoa mhanga kwa kujilipua ili kutimiza jihad, maafundisho ya dini mfu zisizo na msaada kwa roho za watu zinasisitiza taratibu za nje kama kubatizwa, kuzikwa na kiongozi wa dini na sherehe mbali mbali za dini bila mabadiliko ya kweli moyoni .

Yuda anatuhimiza kuweka nguvu zetu katika imani sahihi inayoleta wokovu toka kwa kwa Bwana Yesu. Wokovu ni maisha ya imani yanayoegemea kwa Bwana Yesu na kuongozwa naye. Ni maisha ambayo Yesu Kristo ndio mhimili, maana yake ni mwokozi. Hivyo jina Yesu linaisimamia kazi aliyokuja kufanya hapa duniani. Kama vile Mkulima ni jina la kazi afanyayo mtu anayefukua ardhi na kupanda mbengu na kuzitunza hadi kuvuna mazao, kama vile mwalimu kazi yake ni kufundisha basi mwokozi kazi yake ni kuokoa. Na kwa vile alikuja hapa ulimwenguni ina maana Mungu alipenda wokovu utufikie hapa duniani. Nikisema nimeokoka maana yake Mwokozi Yesu ametenda kazi katika maisha yangu. Yesu asipookoa basi hastahili kuitwa Yesu (Mwokozi)

IMANI KATIKA YESU KRISTO NI MUHIMU SANA.

Tunaweka msisitizo mkubwa katika imani ya wokovu kwa sababu kulingana na 1 Pet 1:6 imani ya wokovu ina thamani sana. Thamani yake inathibitishwa na vipimo vya ubora ambavyo ni majaribu. Imani ya wokovu inavuka majaribuni bila kumwaibisha mwokozi. Kama dhahabu inavyopimwa kwa moto, majaribu pia huipima imani ya wokovu na kuithibitisha.

• Hii ni imani takatifu Yuda 1:20 Imani ya wokovu imebeba upekee wa Mungu. Sifa ya uaminifu, ukweli na haki. Haichanganyi uongo au hila au ukatili katika kumwabudu na mkumfuata Yesu. Imebeba upendo na huruma, uaminfu na usafi. Imani ya wokovu haikubaliani na maisha ya uovu.

• Inatolewa mara moja Yuda 1:3 Biblia hudai Kristo baada ya toleo moja dhidi ya dhambi ameketi (amepumzika).

Waebrania 10:12,26, 33-34 Samson alitengeneza na kujirudi kabisa lakini alipoteza maisha yake pamoja na kisasi cha Wafilisti. Ni vigumu sana kurudi pale ulipokwishafikia na Bwana, gharama yake ni kubwa kurudi mahali uliokuwa kwanza.

Esau alitafuta sana nafasi ya kutubu hakuipata, Yakobo akachukua nafasi yake, naye Yuda Iskariote hakupata tana ile fursa aliyopoteza na usimamizi wake akautwaa mwingine.  

LEO TUNAITWA KUSHINDANIA IMANI KWA SABABU:

1. NI NGAO YA MTU WA MUNGU. Usalama wa mtu Mungu umesimama hapo. Efeso 6:16 Shetani akitaka kudhuru mtu anawinda ngao yake ili kumwondolea ulinzi. Bila ulinzi huna kinga maana kila shambulio litakupata (UKOSEFU WA KINGA YA KIROHO)

2. NDIO MKONO WA KUPOKELEA MEMA NA BARAKA TOKA KWA BWANA Yakobo 1:6,7 Marko 11:24

3. NDIO NJIA (MAISHA YA MTU WA MUNGU) Hatuenedi kwa kuona 2 Wakolosai 5:7

4. NDIYO NJIA PEKEE YA KUMPENDEZA MUNGU. Waebrania 11:6 hapa inaelezwa mfano wa Maisha ya Henoko. Huu ni mfano mzuri wa mtu aliyeishi maisha ya kumpendeza Mungu. Bwana akaenda naye. Wako wapi watakaoenda na Bwana katika nyakati zetu. IKIWA UNATAKA KWENDA NA BWANA KATIKA MAISHA YAKO ITABIDI USHINDANIE IMANI YAKO. Jiunge na watumishi wa Mungu wa nyakati zote kuitetea imani yako.

KUNA ORODHA NDEFU YA MASHUJAA WA IMANI.

Naambiwa Mathayo alitetea imani yake na wokovu hadi akauwa kwa upanga kule Ethiopia.

Marko naye katika kuihubiri imani ya wokovu aliuawa pale Alexandria Misri baada ya kuvutwa na magari ya farasi katika njia za mji.

Luka yule tabibu naye alisimama kidete kwa imani yake hadi akatundikwa katika mti wa mtende pale Ugiriki.

Yohana naye baada ya kushindikana kumwua kwa kumtupa katika mafuta yanayochemka alifungwa katika kisiwa cha Patmos.

Petro alipotishiwa kusulubiwa asipoikana imani ya wokovu aliomba asisulubiwe kama Yesu badala yake yeye awekwe kichwa chini miguu juu. Akauwa kule Roma akiitetea imani yake kwa Yesu.

Yakobo alikatwa kichwa Yerusalem lakini hakuikana imani yake.

Bathlomayo alichunwa ngozi katika mateso ya kujaribu kumfanya aikane imani.

Andrea alikusulubiwa msalabani akiwahubiri waliomsulubu juu ya uzuri wa Bwana Yesu hadi akafa.

Thomas akihubiri imani ya wokovu kule India alichomwa mikuki kule India hadi akafa.

Yuda alipigwa mishale na kufa bila kuikana imani yake,

Mathia alipigwa kwa mawe kisha akakatwa kichwa bila kuikana imani yake.

Barnaba aliuawa kwa kupigwa mawe kule Salonike na,

Paulo akakatwa kichwa na Nero kule Roma, wote hawa wakabaki wakitetea imani yao kwa Yesu.

Mimi pia sikuwahi kupata upinzani kuhusiana na imani hadi nilipookoka.

Paulo vile vile ndipo akasema “wote wapendao maisha ya utauwa wataudhiwa” 2Tim 3:12

HATUWEZI KUIKIMBIA HISTORIA, WALA HATUWEZI KUMBADILI MUNGU AU SHETANI. TUNAWEZA KUBADILIKA SISI.

Ikiwa tutasimama kuitetea imani yetu, ndipo itakapodhihirika kuwa imani yetu ina thamani na ubora wake kufunuliwa.

Mungu akubariki

 

 

RUDI UKURASA WA KWANZA

RUDI MWANZO WA UKURASA HUU