KUOMBEA USALAMA WA TAIFA TANZANIA..

Hesabu 14:5 Ndipo Mose na Aroni, wakaanguka kifudifudi mbele ya kusanyiko lote la Kiisraeli lililokusanyika hapo. 6Yoshua mwana wa Nuni na Kalebu mwana wa Yefune, waliokuwa miongoni mwa watu wale waliokwenda kuipeleleza nchi, wakararua nguo zao, 7wakasema na kusanyiko lote la Kiisraeli wakawaambia, “Nchi tuliyopita katikati yake na kuipeleleza ni nzuri sana sana. 8Ikiwa BWANA anapendezwa nasi, atatuongoza kuingia katika nchi ile, nchi itiririkayo maziwa na asali, naye atatupa nchi hiyo. 9Ila tu msimwasi BWANA. Wala msiwaogope watu wa nchi hiyo, kwa sababu tutawameza. Ulinzi wao umeondoka, lakini BWANA yupo pamoja nasi. Msiwaogope.’’ 10Lakini kusanyiko lote likazungumza juu ya kuwapiga kwa mawe. Ndipo utukufu wa BWANA ukaonekana katika Hema la Mkutano kwa Waisreali wote.

Wakati Mungu alipokusudia kuwaingiza Israel Kanani alimwelekeza Musa kutuma wapelelezi (watu wa usalama) ili wajue jinsi ya kuindea nchi ile. Watu hawa walichaguliwa kwa uwiano wa makabila yote ya Israel (maana ndani ya usalama ikiwemo chembe ya upendeleo wa ukabila au udini tayari hiyo ni udhaifu wa kiusalama).

Kutofautiana kwa Kalebu na Yoshua na wale wapelelezi wengine kumi, na taarifa yao iliyojaa imani kwa Mungu na utii kwa makusudi mema ya Mungu juu ya taifa iliufanya utukufu wa Mungu kushuka. Kusudi baya walilokwisha chochewa watu kuliazimia la kuasi na kuwauwa watumishi wa Mungu na kurejea Misri likasimamishwa.

1.Omba mpasuko mkubwa ndani ya usalama wa taifa katika majukumu (assignment) yote yasiyokuwa na tija kwa wananchi wa Tanzania. Mungu ainue ndani ya usalama kina Joshua na Kalebu ambao watasimamia kusudi jema la Mungu na kuuleta utukufu wa Mungu kwa misimamo na taarifa zao katika taifa letu.

2. Omba moyo wa uzalendo na upendo kwa watanzania kwa watu wa usalama kuliko utii kwa vikundi vya watu wachache wenye maslahi binafsi. Watu kama hao kwa kawaida hupenda kuwatumia watu wa usalama kufanikisha malengo yao binafsi na kutekeleza mipango inayowaondolea haki na maendeleo raia.

2 Samwel 15:10Kisha Absalomu akatuma wajumbe (wapelelezi) kwa siri katika makabila yote ya Israeli, kusema, “Mara mtakaposikia sauti ya tarumbeta basi semeni, “Absalomu ni mfalme huko Hebroni.” 11 Watu mia mbili kutoka Yerusalemu walikuwa wamefuatana na Absalomu. Walikuwa wamealikwa kama wageni nao walikwenda kwa nia njema, pasipo kujua lo lote.

Biblia inaonyesha katika utawala wa Daudi mwanawe Absalom alikusudia kuasi na kuutwaa ufalme wa baba yake. Alichofanya alikula njama na watu wa usalama. Yeye alikulia ikulu alikuwa anawajua vizuri na akatumia fursa ya kuwa karibu nao kujitafutia maslahi binafsi katika ufalme.

3. Vunja mpango wowote uliopa au unaoandaliwa na mtu au kikundi cha watu katika nchi hii wa kuwatumia watu wa usalama kwa maslahi binafsi. Haribu kila hila na ujanja unaoandaliwa (kama aliokuwa nao Absalom katika ufalme wa Daudi) ili kuhujumu na kusaliti wananchi na maendeleo ya nchi ya Tanzania kwa maslahi ya wachache.

Yoshua 2:12 Sasa basi, tafadhali niapieni kwa BWANA, kwamba mtaitendea hisani jamaa ya baba yangu, kwa kuwa mimi nimewatendea hisani. Nipeni ishara ya uaminifu. 13kwamba mtayahifadhi maisha ya baba yangu na mama yangu, ndugu zangu wa kiume na wa kike, pamoja na wale wote walio wa kwao na kwamba mtatuokoa na kifo. 14Wale watu wakamhakikishia Rahabu, “Uhai wetu kwa uhai wenu! Ikiwa hutatoa habari ya nini tunachofanya, wakati BWANA atakapotupa nchi hii, tutawatendea kwa hisani na kwa uaminifu.”

Kulikuwa na wapelelezi wakati wa Yoshua ambao walitumwa Yeriko kabla Israel hawajaenda vitani huko. Watu hawa kulingana na mazingira waliyokutana nayo huko na ombi la Rahabu walifanya maamuzi mazito bila kumshirikisha Yoshua ya kuweka agano na Rahabu aliyewahifadhi hai. Baadaye walipokwisha rudi walimpa Yoshua taarifa na kuweka wazi maamuzi waliyofanya; Yoshua akayaheshima hata ingawa mji wa Yeriko wote ulitakiwa kuwa wakfu kwa Bwana. (Ndiyo maana ulitetekezwa bila kitu chochote kutolewa isipokuwa Rahabu na familia yake, Akani alipojaribu kutoa baadhi ya vitu ilikuwa laana kwake).

4. Ombea watumishi wa kitengo cha usalama wa taifa kuwa na maamuzi thabiti katika mambo yanayohusu usalama wa nchi kwa manufaa ya wananchi wote. Omba Mungu awavike na ujasiri wa kujisimamia katika kazi zao na maamuzi huku wakitunza maadili ya kazi yao na kuheshimu sheria iliyounda chombo hiki. Kataa kabisa watu hawa kutumiwa kama matarishi (au roboti) wasioweza kuhoji sababu, maana na uhalali wa kile wanachoagizwa kufanya. Mungu awavike hekima na kuwapa neema ya kutekeleza majukumu yao kwa faida ya taifa.

5. Omba Mungu akivike heshima chombo hiki machoni pa wananchi wa Tanzania wakipende, kukiombea na kukiheshimu pia kipate heshima machoni pa watawala wakikitumia kwa jinsi inayofaa na kuheshimu taarifa mbali mbali wanazopelekewa. Omba chombo hiki kiwe macho ya watanzania kwa ustawi wa taifa.

 

 

RUDI UKURASA WA KWANZA

RUDI MWANZO WA UKURASA HUU