IJUE VITA YAKO(2)

Kati ya maadui zako wa imani wanaoweza kukufanya ukose mema na kupoteza muujiza wako wa kwanza kabisa ni mashaka.

MASHAKA JUU YA KILE MUNGU ALICHOSEMA (AHADI)

Yakobo 1:

6 Lakini anapoomba, lazima aamini wala asiwe na shaka, kwa sababu mtu aliye na shaka ni kama wimbi la bahari, lililochukuliwa na upepo na kutupwa huku na huku. 7 Mtu kama huyo asidhani ya kuwa atapata kitu cho chote kutoka kwa Bwana. 8 Yeye ni mtu mwenye nia mbili, mwenye kusitasita katika njia zake zote.

Ni shida mtu kupokea chochote ikiwa ana mashaka na uaminifu kwa Mungu. Mashaka yanamfanya Mungu awe kigeu geu au tapeli. Mashaka yanamdhalilisha Mungu. Mungu anakuwa kama vile anasema ovyo, hajui anachosema na wala hakimaanishi. Maneno ya Mungu si maneno ya mwendawazimu, ni maneno imara yasiyotanguka.

Waebrania 6:

13 Mungu alipompa Abrahamu ahadi Yake, kwa kuwa hakuwepo mwingine aliyekuwa mkuu kuliko Yeye ambaye angeweza kuapa kwa jina lake, aliapa kwa nafsi Yake, 14 akisema, “Hakika nitakubariki na kukupa wazao wengi.”

17 Kwa njia hii, Mungu alipotaka kuonyesha kwa udhahiri zaidi kwa warithi wa ile ahadi ile asili ya kutokubadilika kwa ahadi Yake, aliithitibisha kwa kiapo. 18 Mungu alifanya hivyo, ili kwa vitu viwili visivyobadilika, yaani ahadi Yake na kiapo Chake, ambavyo kwa hivyo Mungu hawezi kusema uongo, sisi ambao tumemkimbilia, tuwe na moyo mkuu kulishika lile tumaini lililowekwa mbele yetu.

Mungu alipompa Ibrahim ahadi aliweka na kiapo. Neno la Mungu linaonyesha alitaka kuwapa wale watakaomwamini uhakika kuwa anaweza kufanya yote aliyoahidi. Hivyo kwa mambo mawili yasiyoweza kubadilika yaani ahadi na kiapo sisi tupate faraja sisi tuliomkimbilia Mungu kuwa faraja yetu. Kile Mungu anachosema amefanya tayari amefanya. Kama anasema “ kwa kupigwa kwake (Yesu) mliponywa.” Ina maana ni kweli kabisa tulikwisha ponywa mbele za macho ya haki ya Mungu. Hakuna ugonjwa wowote wenye uwezo wa kutung’ang’ania ikiwa tumesimama katika ukweli huu. Hapa shetani atakachojaribu kufanya ili aweke magonjwa juu yetu ni kututia mashaka juu ya uponyaji huu. Shetani ataleta mawazo ya kuona kama haiwezekani kuwa tayari tumeponywa. Ataleta mawazo ya kuahirisha jambo hili. “Labda siku za mbele upako utakapoongezeka kanisani bila shaka utaponywa. Mungu yupo siku moja atakusaidia.” Haya ni mawazo ya uongo toka kwa shetani. Ukweli unabaki vile vile kwa atakaye uamini “ kwa kupigwa kwake (Yesu) mliponywa.”

Wakati umefika kwa mwenye mashaka kuyatumia mashaka yake vizuri. Hebu tumia uwezo wako wa kutia shaka kwa kutilia mashaka mashaka yako. Mtilie mashaka shetani. Kwa nini umtilie mashaka Bwana Yesu na maneno yake na ushindwe kumtilia mashaka shetani na mawazo ya mashaka anayokuletea? Jisemee kama Daudi “ Sitakufa bali nitaishi” “Aliye pamoja name ni mkuu, kuliko yeye aliye katika dunia”.

TARAJA

Waebrania 11: 1 “Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni udhahiri wa mambo yasiyoonekana.”

Imani ni sasa. Taraja huonekana kama rafiki mzuri. Taraja au tumaini ni kama chui mwenye madoa doa na sura nzuri. Tena kucha zake huzificha ndani ya mfuko wa mkono wake. Lakini ukweli ni kuwa chui ni hatari sana. Taraja huhairisha muujiza wako na kuupeleka katika tarehe za mbele zisizojulikana. Hupotezi tumaini la kupata suluhisho toka kwa Mungu, lakini taraja husema sio leo. Imani inasema ni leo. Mungu anajitambulisha kwetu kuwa yeye ni Mungu wa leo. Ni NIKO AMBAYE NIKO. Kutoka 3:14

Marko 11:23-24.

24 Kwa sababu hiyo nawaambia, yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mmeyapokea nayo yatakuwa yenu.

Huwezi kupata isipokuwa unayo. Biblia husema ili uweze kupokea kitu toka kwa Bwana wakati unaposali uamini kuwa kile kitu ulichokiomba umekipokea kwanza. Ndani ya moyo wako uwe na uhakika kuwa tayari jambo uliloomba umepewa. Kwa imani ushikilie kile kitu mkononi. Uwe na uhakika kuwa unacho. Ndipo biblia husema kitakuwa chako. Utakuwa nacho. Kwa maneno mengine ni kuwa ushinde mashaka juu ya kumiliki kile kitu na pia usiweke umiliki wa hicho kitu siku za usoni. Usiseme Mungu akipenda kitu hiki nitakipata. Useme namshukuru Mungu amenipa kitu hiki na kile. Labda rafiki fulani atasema Oh vizuri sana wewe ni mtu mwenye bahati, je kiko wapi kitu unachoniambia tayari umekipata? Hapo usiseme “kusema ukweli bado sijakipata.” La mwonyeshe ahadi ya Mungu, sema rafiki Mungu amenipa afya yangu pale Yesu alipopigwa mijeledi. Afya ninayo sasa hebu angalia hapa katika 1 Petro 2:24. Namshukuru Mungu sana kwa mapigo yale niliponywa!

Mfano rahisi ni Mariamu na Yesu.

Yohana 11: 21 Martha akamwambia Yesu, ‘‘Bwana, kama ungalikuwa hapa, ndugu yangu hangalikufa. 22 Lakini sasa ninajua kuwa cho chote utakachomwomba Mungu, atakupa.’’

Martha alikuwa anaamini katika uwezo mkuu wa Bwana Yesu, na alijua siri ya nguvu ya maombi aliyo nayo Yesu. Martha ni picha ya wakristo. Watu wanajua Yesu ana uwezo mkuu. Tena watu wanajua siri kuu katika nguvu ya maombi

23 Yesu akamwambia, ‘‘Ndugu yako atafufuka.’’

Bwana Yesu alipoona kauli imara ya Martha juu ya nguvu zake na uwezo wake akamfunulia kusudio lake pale. Hii ni ahadi isiyoweza kutanguka kutoka kwa Bwana Yesu. Tena haina masharti yoyote. Ni ahadi ya moja kwa moja. Ahadi zingine zina masharti, ukifanya hivi itakuwa hivi. Lakini ahadi hii haina sharti lolote. Yesu yupo tayari kutenda jambo kubwa hapa.

24 Martha akamjibu, ‘‘Ninajua ya kuwa atafufuka wakati wa ufufuo wa wafu siku ya mwisho.’’

Unaweza kuona mwitikio wa Martha kwa azma na kusudi la Yesu. Yesu amekwisha weka wazi lengo lake. Martha anapingana na Bwana Yesu kwa kujifanya wa kiroho. Anahairisha muujiza wa ndugu yake kufufuka. Yesu una nguvu lakini hili la Lazaro kufufuka si la sasa. Itakuwa siku ya mwisho. Hili ni taraja au tumaini. Tumaini linaondoa mwujiza sasa na kuupeleka siku ya mwisho. Unaweza kusema haina madhara lakini itabidi Lazaro abaki kaburini hadi wakati huo. Yesu anamwambia Martha huko ni mbali sana. Mimi ndiye huo ufufuo na uzima unaousubiri siku ya mwisho. Niko hapa pamoja nawe sasa hivi, je ni lazima tusubiri siku ya mwisho? Kama unaamini kuwa Lazaro atafufuka na mimi ufufuo na uzima niko hapa tunasubiri nini?

25 Yesu akamwambia, “Mimi ndiye huo ufufuo na uzima. Yeye aniaminiye Mimi, hata akifa atakuwa anaishi 26 na ye yote aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je, unasadiki haya?’’

Unaweza kuona watu wengi wameahirisha miujiza ya Mungu katika maisha yao kwa kusogeza tarehe mbele. Inasikika kama wako kiroho sana. Wanasema najua tu Mungu mwenyewe ndiye atakaye nisaidia. Sina mashaka iko siku Mungu ataniponya. Lakini bado hiyo sio imani. Imani ni sasa, inapokea na kumiliki leo. Kama watu wengi ambao wamengoja kwa uvumilivu miujiza yao wangerekebisha kidogo imani zao ni kuziweka katika hali ya sasa wangepokea haja zao. Imani ni sasa.

 

 

RUDI UKURASA WA KWANZA

RUDI MWANZO WA UKURASA HUU