MAPAMBAZUKO YA SIKU NJEMA.

Dibaji:

Mkononi mwako una ramani itakayokueleza jinsi ya kuendelea katika maisha mapya ndani ya Kristo.

Wataalamu hutuambia mtoto anapozaliwa maziwa ya kwanza anayonyonya kwa mama yana viini lishe na madawa yenye kinga yatakayomsaidia mtoto maisha yake yote. Kijitabu hiki kimebeba msaada kwa mtu aliyempokea Yesu kama Bwana na mwokozi wake. Kama vile mwanadamu anavyoanza maisha mara tu baada ya kuzaliwa duniani wewe pia umeanza maisha mapya baada ya kumpokea Yesu kama Bwana na mwokozi wako. Biblia hutuambia mtu anayempokea Yesu kama mwokozi wake amezaliwa upya katika roho yake. “ Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa roho ni roho. Usistaajabu kwa kuwa nailikuambia, Hamna budi kuzaliwa mara ya pili. Upepo huvuma upendako, na sauti yake waisikia, lakini hujui unakotoka wala unakokwendda; kadhalika na hali yake kila mtu aliyezaliwa kwa Roho.” Yohana 3:6,8

Kijitabu hiki kitakuelekeza jinsi ya kujenga maisha yako juu ya mwamba wa Neno la Mungu katika upendo wa kweli na utakatifu. Unaweza kukisoma peke yako, au pamoja na wenzako katika kundi.

Muhimu:

• Tenga muda maalum wa kusoma kijitabu hiki.(Unaweza kusoma somo moja kila siku)

• Omba kabla ya kuanza ili Mungu akufunulie ukweli na kukuongoza unaposoma.

• Soma kutoka Biblia vifungu vilivyoandikwa ndani ya kijitabu hiki.

• Jibu maswali yote yanayoulizwa kwa jinsi unavyoweza.

• Jadiliana na wenzako katika kikundi au mwulize mtu mwingine aliyeokolewa pale unapokutana na mambo usiyoyaelewa.

Mungu akubariki.

SOMO LA KWANZA

Somo la Utangulizi.

Mpendwa msomaji, maisha ya mwanadamu yanadai maamuzi kila siku ili kufanikisha mipango mbali mbali ya maisha. Uamuzi muhimu kuliko wowote mwandamu anaoweza kuufanya ni ule wa kumpa moyo Bwana Yesu ili autawale. Huu ni uamuzi unaokupa kuchagua kati uzima na mauti. Unapofanya uamuzi ukiwa na akili yako timamu kumpokea Yesu kama mwokozi wako umepita kutoka mautini na umeingia uzimani. Yohana 5:24

Kila mwanadamu anakabiliwa na uamuzi huu muhimu. Hatari ya kupotea milele mbali na uso wa Mungu katika jehanamu ya moto inamwinda kila mwanadamu. Hii ni kwa vile tangu mwanadamu wa kwanza Adamu alipoasi katika bustani ya Eden wanadamu wote waliofuata wamerithi asili hii mbaya ya dhambi na uasi. Hata mwanadamu mzuri kiasi gani katika jamii amebeba asili hii ya dhambi. Hakuna tendo lolote unaloweza kufanya kujinusuru na matokeo mabaya ya dhambi. Jitihada zetu kutenda mambo ya dini kama kuimba kwaya, kusali siku za ibada, kutenda mema na kutoa sadaka haziwezi kubadili asili mbaya ya dhambi ndani yetu. Kwa sababu “…sisi sote tumekuwa kama mtu aliye mchafu, Na matendo yetu yote ya haki yamekuwa kama nguo iliyotiwa unajisi..” Isaya 64:6

Ndiyo maana Mungu Baba yetu mwema wa mbinguni aliamua kutunusuru kwa kumtuma mwana wake Yesu Kristo ili kutuokoa na asili hii mbaya ya dhambi. “ Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa mwana wake wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.” Yohana 3:16.

Wokovu unaoleta uzima wa milele huja katika maisha ya mtu kupitia uamuzi wa mtu binafsi kumkaribisha Bwana Yesu katika maisha yake ili amtawale na kuongoza maisha yake. Hatua hii ndiyo kumwamini Yesu.

“ Bali wote waliompokea (Yesu) aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake;” Yohana 1:12

“ Tazama, nasimama mlangoni nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango , nitaingia kwake,name nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.” Ufunuo 3:20

Hivyo basi uamuzi wako wa kumkaribisha Bwana Yesu ayatawale maisha yako umekuletea uzima wa milele katika maisha yako. Ndiyo maana nakwambia uamuzi huu ni muhimu na wa thamani kuliko maamuzi mengine yote uliyowahi kufanya katika maisha yako.

Mungu akubariki sana.

JIPIME UELEWA WAKO

Je kulingana na Yohana 5:24

1. Je ni mambo gani mawili yanayoweza kumfanya mtu akose uzima wa milele na ahukumiwe?

a………………………………………………………………………………………………

b……………………………………………………………………………………………

2. je wewe binafsi unafikiri umekwisha sikia Neno la Bwana Yesu kuhusiana na wokovu wako na kualimini?

Kama jibu ni ndiyo unakumbuka ni lini na wapi?

3. Kulingana na Isaya 46:6 Mungu anayaonaje matendo yetu ya haki tunayofanya kujaribu kumpendeza?

4. Je Mungu amefanya nini ili kumsaidia mwanadamu katika hali yake ya kupotea? Jibu ukitumia Yohana 3:16.

5. Soma Yohana 1:12 na kujibu; Ili kufanyika mtoto wa Mungu na kupata uzima wa milele unatakiwa kufanya nini?

CHUKUA HATUA

1. Kama hujawahi kumpokea Yesu kwa imani katika moyo wako na ungependa sasa kumpa moyo wako Sali sala hii.

Mpendwa Bwana Yesu, mimi ni mwenye dhambi. Nasikitikia dhambi zangu. Naomba unisamehe. Nafungua mlango wa moyo wangu na kukukaribisha katika maisha yangu. Kuanzia leo ninakukiri wewe kuwa ni Bwana wa maisha yangu.ulikufa msalabani kwa ajili ya wokovu wangu. Ahsante kwa kunipenda. Kuanzia leo nitakutii na kukufuata siku zote sa maisha yangu zilizosalia. Naachana na maisha mabaya na njia za shetani. Katika jina la Yesu Amen.

2. Kama ulikwisha mpokea Yesu siku za nyuma au leo kwa kufuatisha sala hapo juu sasa Chukua fursa hii na mshukuru Mungu kwa maneno yako mwenyewe kwa kukuletea wokovu kwa njia ya Yesu Kristo. Mshukuru Mungu kwa kulifikiisha Neno la wokovu kwako na kukusaidia kuliamini.

 

 

RUDI UKURASA WA KWANZA

RUDI MWANZO WA UKURASA HUU