IJUE VITA YAKO(4)

MATENDO YANAYOPINGANA NA IMANI YAKO

Yakobo 2:

20 Je, wataka kujua, wewe mwanadamu usiye kitu, kwamba imani bila matendo haifai kitu?

Yakobo 2:

21 Je, Abrahamu baba yetu hakuhesabiwa haki kwa kile alichotenda, alipomtoa mwanawe Isaki madhabahuni? 22Unaona jinsi ambavyo imani yake na matendo yake vilikuwa vinatenda kazi pamoja, nayo imani yake ikakamilishwa na kile alichotenda.

Watu wengi hawajui kuwa kinachofungulia mfereji wa imani iliyoko moyoni ni hatua ya imani unayochukua. Imani ni kuchukulia kuwa kitu ambacho Mungu amesema ni sahihi. Na namna unavyoweza kudhihirisha kuwa unachukulia alichosema Mungu kuwa ni sawa; ni kuchukua hatua inayotokana na anachosema Mungu. Ibrahim alipoambiwa na Mungu kutoa sadaka, hakuitikia tu bali aliondoka akamchukua Isaka , akamfunga na kuchukua kisu ili amchinje kama sadaka na kumtetekeza moto. Huo ndio ulikuwa utaratibu wa kumtolea Mungu sadaka nyakati hizo. Alijua sadaka yangu itafika mbele zake na kuuburudisha moyo wake Mungu. Biblia inasema Mungu alimhesabia haki. Maana yake Mungu alichukulia kuwa Ibrahim amempa sadaka ya mtoto wake wa pekee Isaka. (Ingawa kwa ukweli Isaka hakuchinjwa maana Mungu alimzuia)

Unapofanya maungamo ya kiimani ni lazima matendo yako yaoane na kile unachokiri maana hiyo ndiyo imani yako. Shetani mara nyingi atajaribu kuzuia usichukue hatua za kudhihirisha imani yako. Watu wengi wanaamini lakini hawachukui hatua yoyote.

Kijana mmoja kanisani kwetu aliyekuwa ameomba na kukutanishwa na mwenzi wake kwa uongozi wa Mungu alikumbana na upinzani mkubwa ndani ya familia. Muda mwingi aliutumia kuomba na kukiri kuwa Yule binti ni mke aliyepewa na Bwana. (Na kweli ndivyo ilivyo kuwa) lakini miaka ikaendelea kupita bila wazazi kukubali ndoa hii ifungwe. (Kanisani kwetu tunaamini ni muhimu kuwashirikisha wazazi katika kufunga ndoa. Hii ni kwa vile Neno la Mungu linasema mwanamume ataondoka kwa baba yake na mama yake- wazazi, ndipo aende kuungana na mkewe Mathayo 19:5) Baada ya muda kijana alinijia kusema tuombe ili wazazi waridhie ili afunge ndoa na mwenzi wake. Nikamwambia tayari tumekwisha omba sasa ni jukumu lako kuamini. Akaniambia mtumishi wa Mungu mimi naamini. Nikamwuliza tena kama unaamini basi ni lini mtafunga hiyo ndoa? Akafikiri kidogo kisha akasema mwezi Fulani (akautaja). Nikamwambia anza basi maandalizi kwani siku zimebaki chache. Maandalizi yaliendelea na wazazi waliendelea kugoma, lakini kwa vile hii ilikuwa hatua ya imani siku ya arusi wazazi walikuwepo katika sherehe wakifurahi na kupiga vigele gele. Unaona huyu kijana angeweza kuomba miaka mingine mitano kama asingechukua hatua ya kufanya kitu kuhusiana na anachoamini.

Mfano mzuri ni mgonjwa aliyekuwa amelala na imani yake kwa miaka mingi aliyekutana na Yesu.

Yohana 5:

2 Huko Yerusalemu, karibu na mlango uitwao Mlango wa Kondoo, palikuwa na bwawa moja lililoitwa kwa Kiebrania Bethzathaa, ambalo lilikuwa limezungukwa na kumbi tano. 3 Hapa palikuwa na idadi kubwa ya wasiojiweza, yaani, vipofu, viwete, na waliopooza, wakingojea maji yatibuliwe, 4 kwa maana malaika alikuwa akishuka wakati fulani, akayatibua maji na yule aliyekuwa wa kwanza kuingia ndani baada ya maji kutibuliwa alipona ugonjwa wo wote aliokuwa nao.] 5 Mtu mmoja alikuwako huko ambaye alikuwa ameugua kwa miaka thelathini na minane. 6 Yesu alipomwona akiwa amelala hapo, naye akijua kuwa amekuwako hapo kwa muda mrefu, akamwambia, “Je, wataka kuponywa?’’ 7 Yule mgonjwa akamjibu, “Bwana, mimi sina mtu wa kuniingiza bwawani maji yanapotibuliwa. Nami ninapotaka kutumbukia bwawani, mtu mwingine huingia kabla yangu.’’ 8 Yesu akamwambia, “Simama, chukua mkeka wako na uende.’’ 9 Mara yule mtu akapona, akachukua mkeka wake, akaanza kutembea.

Unaweza kuona huyu mtu alikuwa na imani ya uwezo wa Mungu kumponya. Aliamini katika nguvu ya Mungu kuponya mtu kwa mwujiza. Alikaa kando ya Bwawa akiwa na tumaini la kupona siku moja lakini hakupona. Miaka ikapita akiwa katika hali hiyo hiyo hadi alianza kukata tamaa. Alianza kulaumu wagonjwa wenzake walioponywa, akawalaumu jamaa zake wasiomsaidia. Kwa neema ya Mungu Yesu akapita njia ile. Jambo la ajabu Yesu alikuwa na suluhisho rahisi juu ya tatizo hili gumu. “Simama, chukua mkeka wako na uende.’’ Fanya kitu kuhusiana na kile unachoamini. Chukua hatua. Mgonjwa naye hakufanya ubishi kama watu wengine wanavyofanya. Angeweza kusema Yesu kweli huoni hali yangu mimi nina matatizo ya kupooza siwezi kabisa kusimama. Lakini biblia husema 9 Mara yule mtu akapona, akachukua mkeka wake, akaanza kutembea. Je alijuaje amekuwa mzima? Alipoona amesimama na imewezekana. Akachukua godoro lake akaenda zake nyumbani.

Watu wengi wamebaki na imani mioyoni mwao hata wakati mwingine wanakiri mambo sahihi ya kiimani lakini hawaoni matokeo ya imani zao. Shida ni nini? Hakuna matendo ya kiimani yanayoambatana. Wanatenda tofauti na imani. Na hivyo wanabaki katika shida zao.

Shetani angependa watu wasichukue hatua kwani hapo anaweza kuzidhoofisha imani zao.

 

 

RUDI UKURASA WA KWANZA

RUDI MWANZO WA UKURASA HUU