MAPAMBAZUKO YA SIKU NJEMA.

SOMO LA PILI.

WOKOVU NI MPANGO WA MUNGU KWA MWANADAMU.

1. Utangulizi

Siku za leo kuna maswali mengi kuhusiana na wokovu au kuokoka. Wengine huuliza wokovu umetoka wapi? Mambo haya ya kuokoka yameanza lini na yalianzia wapi au yalianzishwa na watu gani. Watu wana majibu tofauti tofauti. Wengine wanasema wokovu ni dini mpya zilizozuka siku hizi za mwisho, wengine husema mambo haya yametokea Marekani na Uingereza nyakati za karibuni, wengine wanasema yameibuka katika nyakati hizi za utandawazi. Je jibu la kweli ni lipi kuhusu wokovu?

2. Ujio wa Bwana Yesu duniani ni chimbuko la wokovu.

“Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao” Mathayo 1:21

Maneno haya aliambiwa Yusufu katika ndoto wakati walipokuwa anafikiri kumwacha Maria kwa vile aligundua kuwa ni mja mzito. Malaika Gabriel alimjulisha Yusufu kuwa mimba hiyo ni mpango wa Mungu. Yusufu aliambiwa mtoto atakapozaliwa aitwe YESU maana yeye amekuja kuokoa watu kutoka katika dhambi. Hivyo jina YESU lilitoka mbinguni kwa mkono wa malaika kuitangaza kazi ya wokovu ulioletwa duniani na Mungu mwenyewe. Jina Yesu maana yake ni mwokozi. Mwalimu hufundisha, dereva huendesha magari, mganga hutibu; mwokozi afanye nini kama si kuokoa watu na dhambi zao?

3. Yesu mwenyewe alitangaza kazi aliyokuja kuifanya duniani.

“Yesu akamwambia, leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahim. Kwa kuwa mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.” Luka 19:9-10

Yesu nyumbani mwa Zakayo, mtoza ushuru mwovu aliyewadhulumu watu fedha zao, alitangaza kuwa ujio wakeumeufikisha wokovu mle. Kutokana na tangazo lake, Yesu alijua jambo lililomleta duniani, kutafuta na kuokoa kilichopotea. Hivyo tunafahamu aliyeleta wokovu duniani sio wanadamu ni Yesu mwenyewe. Sio wamarekani wala wamishionari ni Yesu. Kesi ya kuleta wokovu kwako inapaswa kujibiwa na Yesu.

4. Mitume na wanafunzi wake walitambua kuwa Yesu pekee ndiye anayeokoa.

“Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo” Matendo ya mitume 4:12

Wanafunzi waliotembea na Yesu na kuona aliyoyatenda na kusikia mafundisho yake walifikia hitimisho kuwa ni Yesu pekee anayeokoa. Kazi hii nyeti ya kuokoa mwanadamu ilionekana dhahiri katika huduma Yesu aliyofanya duniani. Mitume hawa ni mashahidi. Kumbe hata wokovu wako bado ni ushahidi kuwa Yesu yuko kazini maana yeye pekee ndiye anayeokoa.

5. Mungu ndiye hutaka watu waokolewe.

“Hili ni zuri, nalo lakubalika mbele za Mungu Mwokozi wetu ambaye hutaka watu wote waokolewe, na kupata kuyajua yaliyo kweli.” 1 Timetheo 2:3,4

Kama kuna anayesukuma na kufuatilia ili watu watu waokolewe basi ni Mungu mwenyewe. Mtume Paulo aligundua kuwa ni Mungu anayetaka watu wote waokolewe. Watu wote ni pamoja na wewe. Mungu anataka watu waokolewe kwa sababu wokovu ni mzuri. Watu wanaweza kusema kuokoka ni kitu kibaya ni kuchanganyikiwa n.k, lakini Mungu anaona ni jambo zuri. Inawezekana watu wengine wasiukubali wokovu. Inaweza madhehebu mengine yasiukubali wokovu, inawezekana baadhi ya viongozi wa dini wasiukubali wokovu, lakini mbele za Mungu wokovu unakubalika. Kabisa. Huo ndio mpango Mungu uliokusudiwa na Mungu kwa wanadamu wote.

Hivyo hongera kwa kuokolewa umeingia katika mpango wa Mungu kwa maisha yako. Hatua hii inakufungulia mipango mizuri ambayo Mungu ameyakusudia maisha yako tangu ulipoumbwa.

JIPIME UELEWA:

1. Soma Mathayo 1:19-21 kisha ujibu maswali yafuatayo kutokana na kifungu hicho. Maana ya jina YESU ni…………………………………………………………………………………………………………

2. Wazo la wokovu lilitoka kwa nani?

a) Yusufu

b) Mariamu

c) Malaika

d) Mungu

3.Kulingana na Luka 19:10

i) Je Yesu alifahamu vizuri kazi aliyokuja kufanya hapa duniani?

ii) Kama jibu lako ni ndiyo je ni kazi gani aliyokuja kufanya?

4. Soma Matendo ya mitume 4:10-12 kisha jibu maswali Kulingana na kifungu hiki je watu wasioliamini jina la Yesu wataokolewa?

5. i. Watu na Mungu nani mkubwa?

ii. kulingana na 1 Timetheo 2:3-4 ni jambo gani lililo zuri na linalokubalika mbele za Mungu?.

iii. unachukua msimamo gani ikiwa unagundua jambo fulani watu hawalitaki lakini Mungu analitaka?

CHUKUA HATUA.

Mshukuru Mungu kuwa wokovu umekufikia na wewe. Mshukuru Mungu kwani yeye ndiye ameleta wokovu kwako.

 

 

RUDI UKURASA WA KWANZA

RUDI MWANZO WA UKURASA HUU