MAPAMBAZUKO YA SIKU NJEMA.

SOMO LA TATU.

JE KUOKOKA MAANA YAKE NINI?

1.Utangulizi

Watu wana mawazo mbali mbali kuhusiana na maana ya kuokoka. Wengine hufikiri kusali kanisa la walokole ndio kuokoka. Wengine hufikiri kuacha tabia fulani fulani mbaya kama ulevi, uzinzi n.k ndiyo kuokoka. Utasikia mtu anamwambia mwenzake, siku hizi umeokoka nini, mbona hubanduki kanisani? Je kusali sana ni kuokoka? Hebu tuangalie Mungu anatundisha nini kuhusu maana ya wokovu. Yako mambo matatu yanayofafanua maana ya kuokoka.

2. JAMBO LA KWANZA KUPOKEA MSAMAHA WA MUNGU BAADA YA KUTUBU KWELI.

“Katika yeye huyo (Yesu) kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake.” Efeso 1:7

Wokovu ni kupokea msamaha wa Mungu ulioletwa hapa duniani na Bwana Yesu. Yesu alikufa msalabani ili kulipa adhabu ya dhambi zako.

“uwafumbue macho yao, na kuwageuza waiache giza na kuilekea nuru, na nguvu za shetani na kumwelekea Mungu, kisha wapate msamaha wa dhambi zao, na urithi miongoni mwao waliotakaswa kwa inani iliyo kwangu mini.” Matendo 26:18

Ili watu waweze kupokea msamaha wa dhambi lazima kwanza wafumbuliwe macho na kujijua ni wenye dhambi. Badala ya kujitetea na kutetea mtindo mbaya wa maisha walio nao,waazimie kwa moyo wote kubadili mwelekeo wa maisha yao. Wawe na mtazamo mpya unaotokana mambo mabaya ya giza (shetani) na kuelekeza mioyo yao kumtii Mungu. Lazima kukataa wazi wazi kuzifuata na kuzitumikia nguvu za shetani na kuamua kutumia maisha yao kumwishia Mungu. Hapa ndipo wanaweza kupata msamaha wa dhambi. Ikiwa mtu ameamua kubadili mwelekeo wa maisha yake kwa uamuzi wa moyoni kuachana na mambo ya dhambi na kutumikia au kutegemea nguvu za shetani basi anapata msamaha wa dhambi zake. Hii ndiyo hatua muhimu inayomfungulia mtu mlango wa wokovu.

3. HATUA YA PILI NI KUMPOKEA YESU KATIKA MOYO ANAYELETA UZIMA WA MUNGU.

“Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake.” Yohana 1:12

Msamaha wa Mungu katika maisha ya mtu hufuta dhambi alizofanya huko nyuma. Lakini ili kuishi maisha ya kimungu lazima asili ya dhambi ibadilishwe na mtu apate maisha mapya ya Mungu.Kumpokea Yesu kunaleta uzima wa Mungu ndani yako. Tunashirikiana na Mungu maisha yake. Badala ya kuishi na nguvu, akili na maisha yetu, tunaishi na uzima wa Mungu. Uzima huu huitwa uzima wa milele.

“ Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa mwana wake wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.” Yohana 3:16.

Kutokana na upendo wa Mungu katika maisha yetu, alimleta Bwana Yesu ili tuweze kushiriki uzima wake. Haitoshi kusafishwa dhambi, ili kuishi kama Mungu anavyotaka lazima tuwe na uzima toka kwa Mungu. Uzima wa Mungu hutupa asili mpya ya kiMungu inayoshinda dunia na majaribu yake. Hivyo kuokoka ni kumpokea Yesu katika moyo wako na kuupata uzima wa Mungu. Na kumpokea Yesu kunaleta uzima wa Mungu aktika maisha yako

4. JAMBO LA NNE KUOKOKA NI KUHAMISHWA TOKA UFALME WA SHETANI NA KUINGIZWA KATIKA UFALME WA MUNGU.

“Naye alituokoa katika nguvu za giza, na akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa mwana wa pendo lake;” wakolosai 1:13

Kuna falme mbili zinazopingana na kila mtu ni raia katika mmojawapo wa falme hizi. Kuokoka ni kuondolewa katika ufalme wa giza (shetani) na kuhamishiwa katika ufalme wa Mungu. Unakubali kutubu na kumwelekea Mungu si tu unasamehe dhambi lakini pia unahamishwa na kuingizwa katika ufalme wa Bwana Yesu (mwana wa pendo la Mungu) ikiwa umeokoka huna haja tena na msaada wa shetani katika maisha yako. Hirizi, utabiri na nyota, mapicha mabaya ya uasherati, mazindiko, ibada za mizimu za kimila pamoja na zana za ibada huvihitaji tena. Ulipotubu umebadili msimamo na mwelekeo wako hivyo unayaondoa vitu hivi katika maisha yako maana wewe si raia wa ufalme wa shetani hata ukautii na kuutumikia. Yesu ndiye mfalme wako na anawajibika kukulinda.

HITIMISHO

Mambo hayo matatu hapo juu yanaungana pamoja kutupa maana ya kweli ya kuokoka. Mtu asiyekuwa na hayo hata kama ana sifa ambazo watu na madhehebu wanazikubali bado hajaokoka. Kuokoka si kuja mbele na kuombewa juu ya hitaji fulani kama ugonjwa, mahitaji ya maisha n.k Kuokoka ni kutubu na kupokea msamaha wa dhambi, kumpokea Yesu moyoni anayeleta uzima wa Mungu na kuhamishwa toka ufalme wa giza hadi ufalme wa Bwana Yesu.

PIMA UELEWA WAKO.

1. Je kabla ya somo hili wewe ulikuwa unafikiri wokovu maana yake ni nini?

2. Taja mambo matatu ambayo kwa pamoja yanaeleza maana ya kuokoka.

i……………………………………………………………

ii……………………………………………………

iii………………………………………

3. ikiwa mtu hajaamua kuacha maisha ya dhambi anaweza kupata msamaha wa dhambi ikiwa ataungama mambo aliyokesea zamani? (Soma Matendo 26:18)

4. Soma Yohana 1:12 je uwezo wa kufanyika mtoto wa Mungu unatoka wapi?

5. Unafikirije, Je mtu akipewa uwezo na Mungu anaweza kuokoka?

CHUKUA HATUA.

1. Ikiwa ulikuwa na vitu hivi mtafute mchungaji au mtu aliyeokoka, mweleze ukweli kisha mshirikiane kuomba na kuharibu zana hizi za shetani kama hirizi, mazindiko, picha chafu za mapenzi, vitu vya ibada za mizimu n.k

2. Mshukuru Mungu kwa kukusamehe dhambi zako, kukupa uzima wake na kukuhamisha toka ufalme wa shetani akakuingizia katika ufalme wake.

 

 

RUDI UKURASA WA KWANZA

RUDI MWANZO WA UKURASA HUU