MAPAMBAZUKO YA SIKU NJEMA.

SOMO LA NNE.

JE NI KITU GANI KINATOKEA MTU ANAPO OKOKA?

1. Utangulizi

Bila kujali wewe unavyojiona au kufikiri baada ya kuookoka ni vizuri uchukue mtazamo wa Mungu.

Katika somo hili utagundua mambo 6 ambayo yamefanyika katika maisha yako ulipotubu na kumpokea Yesu.

2. DHAMBI ZAKO ZIMESAMEHEWA.

“Kama mashatiki ilivyo mbali na maghatibi , Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi.” Zaburi 103:12

“Haya njooni, tusemazane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapo kuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu.” Isaya 1:18

Hakuna dhambi yoyote ambayo baada ya kuokoka haiwezi kusamehewa na Mungu. Hata kama ni mbaya sana, tunapotubu na kumpokea Yesu tunasamehe dhambi zote. Unasimama mbele za Mungu ukiwa safi bi la hatia yoyote. Usikubali mawazo yako kutumiwa na shetani kukudanganya kwamba dhambi zako za zamani bado zipo. Hata watu wasikuhukumu kwa yale uliyotenda zamani maana umesamehewa ulipompokea Yesu Kristo.

“ambaye katika Yeye (Yesu Kristo) tuna ukombozi yaani msamaha wa dhambi.” Wakolosai 1:14

3. UMEKUWA KIUMBE KIPYA.

“Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.” 2 Wakorintho 5:17>

Mwanadamu ni roho, inayokaa ndani ya nyumba inayoitwa mwili. Unapompokea Yesu uumbaji mpya unafanywa ndani ya roho ya mtu. Unazaliwa upya kama kiumbe kipya. Unazaliwa na Mungu ukiwa na uzima na asili mpya ya Mungu. Mambo ya zamani hayakuhusu kwani wewe ni kiumbe kipya. Ni kama vile mtu anapohamia nyumba mpya halazimiki kuishi maisha aliyokuwa nayo mpangaji aliyeondoka. Wewe ni mpangaji mpya, mwili ni ule ule lakini mtu (roho) imekwishafanywa upya).

4. WEWE NI MTOTO KATIKA FAMILIA YA MUNGU.

“ Bali wote waliompokea (Yesu) aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake;” Yohana 1:12

Kama alivyo mtoto kwa baba yake ndivyo ulivyo mbele za Mungu. Unazao haki za mtoto katika familia. Mungu ni baba yako na watoto wengine wa Mungu (waamini) ni ndugu zako. Una haki ya kupendwa na Mungu, unahaki ya kutunzwa na Mungu, ulinzi wako hauwategemei wanadamu Mungu anakulinda, una haki ya kurithi katika nyumba ya baba yako. Wakati watu wengine wanatetemeka na kuogopa kumkaribia Mungu wewe unaweza kumwendea kama Baba yako.

“Basi tangu sasa ninyi si wageni wala wapitaji, bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu.” Waefeso 2;19

5. JINA LAKO LIMEANDIKWA MBINGUNI.

Biblia hutufundisha kuwa kuna kitabu cha uzima ambacho wote waliandikwa humo wataingia katika mbingu mpya aliyoandaa Mungu kwa ajili ya watoto wake. “ Na iwapo mtu yeyote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto” Ufunuo 20:15 Ulipompokea Yesu jina lako limeandikwa katika kitabu hiki.

“…bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni. Saa ile ile akashangilia kwa Roho Mtakatifu, akisema, Nakushuru, baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya umewaficha wenye hekima na akili; ukawafunulia watoto wachanga….” Luka 10:20-21

Jina lako limeandikwa mbinguni kwa sababu wewe sasa ni mtoto wa Mungu.

6. UMEHESABIWA HAKI NA MUNGU.

“kwa sababu wote wamtenda dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu; ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake, kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa Mungu dhambi zote zilizotangulia kufanywa; apate kuonyesha haki yake wakati huu, ili awe mwenye haki na mwenye kumhesabia haki yeye amwaminiye Yesu.” Warumi 3:23-26

Kuhesabiwa haki maana yake ni kuonekana kuwa huna hatia mbele ya Mungu. Huna kesi, hivyo una kibali mbele zake.

7. UNA MAMLAKA JUU YA SHETANI.

“Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui , wala hakuna kitu kitakachowadhuru” Luka 10:19

Kuna kitu kinachosababisha wewe sasa uwe na uwezo/ nguvu dhidi ya shetani na kazi zake. Sio sifa ya kibinadamu wala cheo katika kanisa. Yesu alisema ni kwa sababu jina lako limeandikwa mbinguni. “ Lakini msifurahi kwa vile pepo wanavyowatii; bali mfurahi kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni. Luka 10:20 Wakati wowote mahali popote unaweza kulitumia jina la Yesu kuvunja kazi za shetani na kumpinga naye atakimbia.

JIPIME UELEWA.

1.Orodhesha mambo matano ambayo yamekutokea ulipompokea Yesu kama Bwana na mwokozi wako.

i…………………………………………………………

ii…………………………………………………………

iii………………………………………………………

iv………………………………………………………

v…………………………………………………………

CHUKUA HATUA

Mshukuru Mungu kwa kila jambo moja moja hapo juu na kukubaliana ukilitaja neno la Mungu linalokuhakikishia jambo hilo. Mfano: Mungu wa mbinguni nakushukuru kwa sababu kulingana na 2 wakorintho 5:17 mimi (Stella) sasa ni kiumbe kipya. Nimezaliwa na Mungu na ninao uzima mpya toka kwa Mungu. Mambo yote ya kale yamepita. Ahsante Bwana Yesu maana mimi sasa ni kiumbe kipya.

 

 

RUDI UKURASA WA KWANZA

RUDI MWANZO WA UKURASA HUU