MAPAMBAZUKO YA SIKU NJEMA.

SOMO LA TANO.

UNAJUAJE KUWA UMEOKOKA?

1.Utangulizi

Mara nyingine baada ya kuokoka mtu huanza kupata mashaka kama kweli kabisa ameokoka. Hali hii inaweza kusababishwa na mabadiliko katika hisia za mtu, kama alikuwa na furaha sana lakini baadaye furaha ikaodoka. Wakati mwingine watu wanaomzunguka wanapomkatisha tamaa na kumwambia hajaokoka. Somo hili linajibu swali muhimu linaloulizwa mara nyingi, NITAJUAJE KUWA KWELI NIMEOKOKA? Kuna mambo kadhaa yanatupa uthibitisho kuwa sasa tumeokoka.

2. UTHIBITISHO WA NENO LA MUNGU.

Neno la Mungu lina uhakika wa 100% kuwa kila linachosema ndio ukweli. Halikosei wala kugeuzwa. Biblia hutuambia kuwa “Ndipo Bwana akaniambia, umeona vema, kwa maana ninaliangalia neno, ili nilitimize.” Yeramia 1:12 Unajua mbingu na nchi zitapita lakini neno la Mungu halitapita kamwe.

“EE Bwana, neno lako lasimama imata mbinguni hata milele.” Zaburi 119:89 Neno la Mungu hutupa uhakika juu ya wokovu wetu. Ikiwa tunaweza kupata uthibitisho toka neno la Mungu basi huo utatupa uhakika wa kweli juu ya wokovu wetu.

i. Warumi 10:9-10 “Kwa sababu, ukimiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwakao ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu , utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu”

Ina maana kama mtu ameamini kwa moyo wake kuwa Yesu alikuja kulipa deni la dhambi zake, na tena alikufa na kufufuka kwa ajili yake; kama umechukua hatua ya kumkiri kama Bwana na mwokozi wako basi umeokoka.

ii. “ Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa mwana wake wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.” Yohana 3:16.>

Tuna uhakika kuwa kama mtu amemwamini Yesu ana uzima wa milele. Yohana 1:12

iii. “ Bali wote waliompokea (Yesu) aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake;” Yohana 1:12

Kama umempokea Yesu moyoni mwako kwa imani basi wewe ni mtoto wa Mungu.

Yohana 5:24 “Amini, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yey aliyenipeleka una uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani.”

3. AMANI MOYONI.

“Basi tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani, na mwe na amani kwa Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo” Warumi 5:1

Mtu ambaye hajasamehewa dhambi zake anajisikia mwenye hatia mbele za Mungu. Hana ujasiri wala amani na Mungu. Ni kama mtu aliyemkosea mtu anavyosikia vibaya anapokutana na huyo mtu. Lakini pale dhambi zinaposamehewa, ukuta uliokuwepo kati ya mtu na Mungu unaondoka. Unasikia huru mbele za Mungu pasipo hatia. Hii ndiyo hali inayoleta ushwari moyoni, unajisikia vizuri mbele za Mungu. Huu ni uthibitisho kuwa dhambi zako zimesamehewa.

“Sasa basi hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu” Warumi 8:1

4. IMANI KATIKA JINA LA YESU.

“Nimewaandikia ninyi mambo hayo, ili mjue ya kuwa mna uzima wa milele, ninyi mnaoliamini jina laMwana wa Mungu. 1 Yohana 5:13

Mtu anapompokea Yesu na uzima wa Mungu ukaingia ndani yake ghafla anaanza kuliamini zaidi jina la Yesu. Mtu anaona jina la Yesu linaweza kumtetea na kumshindia katika mambo mbali mbali. Anaondoa tumaini lake kwingine na kuwa na uhakika kuwa kuna msaada katika jina la Yesu. Wakati wengine wanakimbilia kwingine mfano kwa waganga, yeye anatupa madawa na kuondoa mazindiko huku akiamini kuwa bado atabaki salama kwa nguvu za Mungu. Huu ni ushahidi kuwa mtu huyu ANAO UZIMA WA MILELE NDANI YAKE.

5. UPENDO KWA WATU WALIOKOKA.

“Sisi tunajua ya kuwa tumepita toka mautini na kuingia uzimani, kwa maana twawapenda ndugu. Yeye asiyependa akaa katika mauti. Kila amchukiaye ndugu yake ni mwuaji, nanyi mnajua ya kuwa kila mwuaji hana uazima wa milele ukikaa ndani yake” 1 Yohana 3:14-15

Mtu anapompokea Yesu anazaliwa katika familia ya Mungu. Tangu hapo anaanza kujisikia kuwa mmoja miongoni mwa watu wa familia ya Mungu. Watu wengine waliokoka wanaanza kuwa wa maana kwake. Unajisikia kuwapenda na kuwaheshimu. Kukutana na kushirikiana nao inakuletea furaha. Hii ni dalili kuwa WEWE SASA UKO KATIKA FAMILIA YA MUNGU.

6. KUCHUKIA DHAMBI..

“atendaye dhambi ni wa Ibilisi, kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo…Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu,” 1 Yohana 3:8-9

Mtu akiokolewa anahamishwa toka himaya ya shetani na hapo mambo maovu ya dhambi yanapoteza maana na utamu kwa mtu aliyempokea Yesu. Ghafla anaanza kuchukia kutenda dhambi. Jambo lolote ambalo mtu analigundua kuwa sio sahihi mbele za Mungu analiacha. Hata pale ambapo kwa ujinga au sababu yoyote mtu anajikuta ametenda dhambi jambo hili linamuumiza moyoni. Mtu aliyeokoka haoni tena raha ya kubakia na dhambi, lazima atafute namna yoyote ya kuondoka nayo kwa njia ya toba. Hii ni dalili kuwa shetani amepoteza uwezo juu ya maisha ya mtu huyu. Amehamishiwa katika ufalme wa mwana wa pendo la Mungu.

7. USHUHUDA WA MOYONI.

“ Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu.” Warumi 8:16 Roho mtakatifu husema ndani ya roho zetu na kuthibitisha kuwa sisi tu watoto wa Mungu. Ni vigumu wakati mwingine kueleza kwa maneno jinsi anavyoongea lakini ujumbe wake huwa tunaupokea ndani sana ya mioyo yetu. Mara tunakuwa na uhakika moyoni kuwa Mungu ametusamehe na tumeokolewa. Hii ni kwa sababu toho mtakatifu hushuhudia ndani ya roho zetu. Uhakika huu si wa kujitungia, tunafuatisha kile tulichosikia toka kwa Roho Mtakatifu,

PIMA UELEWA WAKO.

1. Kulingana na zaburi 119:89 neno la Mungu linaweza kuwa na makosa?

2. Je ikiwa neno la Mungu linasema kitu tufouti na jinsi ninavyojisikia itakuwa sahihi kufuata neno la Mungu au hisia zangu? Soma Matendo ya mitume 5:36

3. Kulingana na Warumi 5:1 amani ya kweli inatokana na………………………………………………………

4. Mtu anapookoka na akaanza kuwapenda watu waliokoka na kujisikia vizuri kushirikiana nao mambo ya Mungu hii inaweza kumaanisha nini?

5. Je mtu aliyeokoka anafurahia kutenda dhambi? Soma 1Yohana 3:8,9

CHUKUA HATUA

1. Kubaliana na neno la Mungu katika Warumi 10:9, 10 kisha mshukuru Mungu kuwa neno hilo limetimia katika maisha yako.

Mfano wa sala unayoweza kutumia:- Bwana Yesu kulingana na Warumi 10:9-10 nimekukiri kwa kinywa changu kuwa wewe ni Bwana wa maisha yangu. Naamini kwa moyo wangu wote kuwa, ulikufa kwa ajili ya dhambi zangu na ulifufuka; huo ulikuwa ni ushindi kwa ajili yangu. Kwa sababu hiyo nimeokoka. Ahsante Bwana Yesu kwa ajili ya wokovu katika maisha yangu. Amen.

2. Kubaliana na neno la Mungu katika Yohana 1:12 kisha mshukuru Mungu kuwa neno hilo limetimia katika maisha yako.

3. Mpe ahadi Mungu kulingana na 1 Yohana 3:9 kuwa hutaambatana na dhambi kwa kukusudia au kuitetea mahali popote katika maisha yako. Ahadi kuwa unatangaza uadui na dhambi katika maisha yako. Omba Mungu akusaidie siku zote kuichukia na kuikataa.

4. Kulingana na 1 Yohana 3:14-15 Waombee Baraka watu wote waliompokea Yesu popote duniani. Kiri kuwa hawa ni ndugu zako katika familia ya Mungu. Mwahidi Mungu kuwapenda.

 

 

RUDI UKURASA WA KWANZA

RUDI MWANZO WA UKURASA HUU