KUUKUBALI MWAKA 2010 NA WIMBO

Huu ni mwaka ambao Mungu anataka tujenge mahusiano yetu na yeye na tutakayowezeshwa kufanya mwaka huu yatakuwa sio ya kusimuliwa. Mungu anataka tufikie mahali ambapo tutakuwa tumejenga uhusiano mzuri na yeye. Huu ni mwaka wa kumkaribia Mungu ni mwaka ambao tutatoka na neno ambalo Mungu amelikusudia katika maisha yetu.

Agalizo: msisitizo ambao Mungu ameuweka katika mwaka huu ni hatua ya imani na kuabudu. Katika mwaka huu tutamfahamu Mungu kibinafsi ni mwaka ambao kila mtu anatakiwa afunge mkanda kuonana na Mungu wake kibinafsi. Enoko katika agano la kale alikuwa kielelezo cha kumfahamu Mungu. Mungu alimuweka ili awe kielelezo cha sisi kumfahamu yeye (Mungu) Mwanzo 5: 21-24

Enoko alitembea pamoja na Mungu ingawa alikuwa na mke na watoto alijenga ushirika na mahusiano ya karibu na Mungu. Na baadaye Mungu alimtwaa alitoweka akaenda na Mungu). Ebrania 11:5-6

Enoko alibadilishwa ghafla kutoka katika mwili huu wa kawaida akawa na mwili wa utukufu akatwaliwa na Mungu kwa sababu alimpendeza Mungu. Kwa vile Enoko alikuwa amejipanga vizuri na Mungu, Mungu aliona amtwae bila kuonja mauti. Kabla Enoko hajaondoka alikuwa ameshuhudiwa kwamba amempendeza Mungu. Alikuwa na ushirika mzuri na Mungu, alikuwa amejenga ule ushirika vizuri na Mungu mpaka akafikia mahali Mungu akaona amtwae bila kuonja mauti. Kitu kilichomfanya Enoko ampendeze Mungu ni ushirika na Mungu. Tunatakiwa tujipeleleze binafsi ushirika na Mungu ukoje?

Kitu chenye nguvu ni ufunuo. Kwa kadri tunapata ufunuo toka kwa Mungu tunazidi kusogea toka utukufu hadi tukufu. Tunahitaji kuwa na Mungu ambaye tumekutana naye sio wa kusimuliwa. Mungu anatutaka katika vyumba vya ndani. Ili yote tuyafanyayo yatokane na yeye. Yoyote tufanyayo kama hayatokani na nguvu iliyo katika Mungu mwenyewe ni bure.

Mungu anataka tujenge mahusiano ya kweli na yeye. Tukiwa na ushirika na Mungu tutabadilika.

Mungu anatuita katika vyumba vya ndani kwa sababu kuna uwezekano wa kusababisha mabadiliko. Imetosha vile tumemjua Mungu kupitia kwa wote wengine. Mungu anatuita katika vyumba vya ndani. Tuwe na jitihada zetu binafsi za kumtafuta Mungu.

Tumefikia wakati ambao tunatakiwa tumfikirie Mungu zaidi. Ni muhimu zaidi kumfurahisha Mungu kuliko kuwafurahisha wanadamu na kumhusisha Mungu. Enoko aliupendeza moyo wa Mungu na ndio maana hakuonja mauti.

Ebrania 11.6 Pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu. Kabla Mungu hajajidhihirisha kwako ni lazima kwanza utumie imani yako. Mungu huwapa thawabu wale wamtafutao. Wale wanaoweka jitihada zaidi kumtafuta, Mungu hawezi kuwatupa. Mungu ana kitu chema kwa wale wamtafutao.

Tukiamini kwamba Mungu yeye ndiye awezaye yote tutamwendea. kwa mfano Mwanamke aliyetokwa damu alifanya kila jitihada ili amfikie Yesu apate msaada, maana alijua kwa Yesu upo msaada.

Mtu akijua kwamba Mungu yupo na kwamba anawatendea mema wale wamtafutao lazima naye atamtafuta. Hakuna kinachoharibika ukimtafuta Mungu, Mungu mwenyewe ataboresha mambo yako.

Daniel 11:32b Watu watakao mtafuta Mungu watakuwa na nguvu (hodari) na watatenda mambo makuu. Ndio watakao badilisha mambo yaliyopotoka watasababisha mabadiliko makubwa. Mwaka huu wa 2010 ni mwaka ambao fursa nyingi zitatokea katika maisha yetu. Pengine vikwazo na matatizo vinaweza kuwa ndio fursa za Mungu kwetu. Kwa hiyo inategemea wewe umejipanga vipi na Mungu.

Fursa zinapotokea ukiziangalia kwa macho ya kibinadamu utaona ni milima. Mfalme Yehoshafati aliona kila mara Baba yake alipokuwa na uhusiano mzuri na Mungu mambo yake yalifanikiwa kwa hiyo aliamua kumfuata Mungu wa kweli.

2 Mambo ya Nyakati 17:1 Kile anachokiona kama mlima ndio fursa yenyewe. Yehoshafati alitawala kwa gia kubwa ya Bwana na Mungu aliusimamisha ufalme wake, akauthibitisha utawala unaomtegemea yeye. Ukiamua kuusimamisha ufalme wa Mungu katika utawala, Mungu anauthibitisha huo utawala.

2 mambo ya Nyakati 20:1,3-6 Watu waliojifunza namna ya kumtafuta Mungu majaribu yakija mahusiano yao na Mungu yanaongezeka. Mfalme Yehoshafati alipoogopa alielekeza uso wake kwa Mungu. Yuda yote walikusanyika na kumlilia Bwana kwa amri aliyoitoa mfalme Yehoshafati.

Mithali (14-17) Mungu aliwahakikishia Israel kwamba atawapigania lakini Israel waende vitani naye ataenda pamoja nao. Mungu anatusubiri twende pamoja naye vitani kwenye majaribu sio yeye apigane peke yake lazima na sisi tusikae. Ukijua kitu Mungu anasema na maisha yako unakuwa umepata mtaji. Tunatakiwa kujua Mungu anasema nini katika majaribu na mambo tunayoyapata maishani mwetu.

Lazima ujue Mungu anasema nini juu ya uchumi wako pia. Kanuni ya uchumi katika ufalme wa Mungu ni kama unataka Mungu ajifunue katika maisha yako kiuchumi lazima ujifunze kutoa sadaka kwa furaha. Ni kwa faida yetu kumshirikisha Mungu mapato yetu. Ni lazima tujue Mungu anasema nini katika afya, masomo, uchumi n.k na tukishajua Mungu anasema nini tuamini nasi tutaona mabadiliko. Israel walipomsifu Mungu kwenye uwanja wa vita Mungu alijifunua kwao. Tutakapoona msaada wa Mungu katika majaribu hata majaribu yenyewe yataanza kukimbia. Ebu angalia adui amesimama upande gani katika maisha yako. Inawezekana hapo hapo unapopatazama kama kitisho ndio bonde la baraka

SISI NDIO MAWAKALA WA KUSABABISHA MABADILIKO.

Muujiza wa Mungu upo wakati wote pindi unapokwenda kwake ni rahisi kumwona au kumpata bila kufanya miadi (appointment) yoyote. Tunapojifunza kutumia siri ya maombi tunaweza kusababisha mabadiliko. Mabadiliko yanayotokea katika uongozi wa kitaifa ni ishara mahususi katika ulimwengu wa roho.

Yeremia 15:1 Hapa Mungu alimwambia Yeremia kwamba hata wangesimama mbele zake Musa na Samweli kuomba moyo wake usingebadilika kuwaelekea watu. Mungu abadilishwi na maombi bali maombi yanatubadilisha sisi na mazingira tuliyomo. Yeremia 14:7-9,11,17-22

Hapa Yeremia alikuwa akimuomba Mungu mvua. Ili tuweze kuomba maombi tunatakiwa tujue kwanza moyo wa Mungu umeelekea wapi (umeangalia wapi) Ili Mungu aweze kuiponya nchi ni lazima kwanza Kanisa lipone. Maombi yanatakiwa kwanza yambadilishe kwanza muombaji halafu ndipo yatabadilisha matukio ila hayawezi kumbadilisha Mungu. Yeremia alipojua moyo wa Mungu umeelekea wapi alibadilika badala ya kuja na hoja za nguvu alikuja na hoja za Mungu.

Yeremia 15:10-11 Yeremia alianza kufanya maandalizi kwa ajili ya kile kilichokuwa kinakuja mbele yake baada ya kujua moyo wa Mungu umeelekea wapi. Tunatakiwa kuuona kwanza moyo wa Mungu tunapotaka kuomba kama hatujaangalia muelekeo wa Mungu basi tutakuwa tunafanya kazi bure. Ukitaka kuona nguvu ya mwombaji pandia kwenye mgongo wa Mungu.

Daniel 9:1-3 Daniel alitulia kwa Mungu akatafuta kwenye vitabu vya zamani vya manabii akagundua maneno yaliyoandikwa na nabii Yeremia akahesabu muda na akaanza maombi ya kuomba toba. Daniel alijibiwa kwa sababu aliomba kwa wakati anaojua. Yeremia aliomba sala ile ile aliyoomba Daniel lakini hakujibiwa kwa sababu ulikuwa sio wakati unaofaa kuomba maombi hayo. Watu walioomba na kupata majibu walikaa kwanza na Bwana na kuujua moyo wake umeelekea wapi.

Ukishajua moyo wa Mungu ulikoelekea hapo ndipo uombe. Huduma ya maombi na maombezi ni huduma ya kinabii kwa sababu unatakiwa kwanza usikilize Mungu anasemaje na ndipo uombe.

1Yohana 5: 14-15 Ujasiri tulionao kwenye maombi ni kwa sababu tumejua lililo kusudi la Bwana katika maombi hayo. Ni muhimu sana kujua kwanza msimamo wa Mungu ni nini katika jambo unalotaka kuliombea.

Yohana 15: 7 "Ninyi mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu ombeni." Kama maneno ya Bwana yakikaa ndani yetu tuombe lolote naye atafanya.

Isaya 43:26 Tukiyajua mapenzi na makusudi ya Mungu basi (Tuombe tumkumbushe naye atafanya) Lazima ujue moyo wa Mungu umeelekea wapi katika yale unayoyaombea.

Marko 11:23:24 Mungu huwa anaheshimu maombi ya mtu anaye amini maombi yake mwenyewe. Kama unaamini kwamba vile ulivyoomba ni sawa sawa na mapenzi ya Mungu basi Mungu atafanya.

Katika tatizo lolote ulilonalo nenda kwenye neno la Mungu na ujue kusudi la Bwana ni nini juu ya tatizo ulilo nalo. Unapoingia kwenye maombi usiangalie tena shida yako bali omba kwa kuangalia msimamo wa neno la Mungu juu ya hiyo shida. Ukisha jua msimamo wa Mungu basi na wewe ufanye uwe ndio msimamo wako kwa maana kuamini kunakuja kabla ya kupokea. Tunatakiwa kujua Mungu anawaza nini kwa kujifunza kurudi katika vyumba vya ndani na kuweka uhusiano wetu na Mungu na tumsikie. Kwa maana tunatakiwa kusikia kutoka kwa Bwana.

 

 

RUDI UKURASA WA KWANZA

RUDI MWANZO WA UKURASA HUU