HUDUMA YA UINJILISTI

Huduma hii kwa sasa hufanyika katika maeneo ya mkoa wa Kagera, hususani mji wa Bukoba na vitongoji vyake ambako kumeundwa timu ya kuhubiri katika maeneo mbalimbali. Hii ni katika kutimiza neno la Bwana na mwokozi wetu Yesu Kristo kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Mathayo 28:19-20.

UNJILISTI KATIKA MAENEO MBALI MBALI YA MJI WA BUKOBA.

Wainjilisti katika huduma hii ni watu waliookoka wanaoshirikiana na huduma ya UCF ( Unity Christian Fellowship) na walio na kiu na wito wa kumtumikia Mungu katika eneo hili la uinjilisti, na hawa wamekuwa wakihubiri katika mitaa mbali mbali ya mji wa Bukoba na vitongoji vyake.

Huduma hii inalea vipawa vya watu walio na wito katika eneo la uinjilisti na wengi wameonyesha kuipenda na kuinua vipawa vyao vya kuhubiri. Zoezi la kuhubiri linaendelea katika mji wa Bukoba na vitongoji vyake kila mara kuanzia saa 9 mchana hadi saa 12 jioni. Na tayari huduma hii imefanyika katika maeneo ya Nyamkazi mwaloni ,Nyakanyasi, eneo la Hamugembe, Mjini kati, Rwamishenye, Buyekera, Migera, Kashai, uzunguni, mashuleni na Omukigusha. Tumeshuhudia watu wengi wakiokoka na kumrudia Mungu.

Bonyeza hapa kufuatilia ratiba ya uinjilisti na huduma zingine katika mji wa Bukoba na Tanzania katika kipindi chote cha mwaka huu wa 2010 na ungana nasi katika kuombea huduma hii, na pia kutusaidia katika kuhubiri katika maeneo hayo pamoja nasi, na kuwalea wale waliookoka, ili wasirudi nyuma tena.

UNJILISTI KWA WAGONJWA HOSPITALINI.

Mahubiri pia yamekuwa yakifanyika katika Hospital kuu ya Mkoa wa Kagera ya Bukoba ikiwa pamoja na maombezi kwa wagonjwa na kuwapa mahitaji muhimu kama sabuni za kuogea na kufulia, juice na mahitaji mengine mbalimbali. Huduma ya hospitali imehitajika sana kiasi ambacho watu wengi wameomba kutembelewa mara kwa mara. Wagonjwa wengi wamekuwa wakitoa maisha yao kwa Bwana Yesu na wengi wakipona kwa kipindi kifupi kutokana na maombezi waliyofanyiwa; kwani baada ya kurudi kuwatembaelea siku zinazofuata hatuwakuti wakiwa hosptalini tena. Hii inathibitisha kwamba maombi ya uponyaji huwa yamefanya kazi tayari.

UNJILISTI KATIKA MAENEO MBALI MBALI YA KAGERA

Mwaka 2003 mnamo mwezi wa June huduma hii ilifanya kampeni ya kupambana na UKIMWI katika mkoa wa Kagera. Kwa kushirikiana na makanisa mbali mbali, Life Ministry na Nehemia Aid Foundation; timu ya watu kama 80 ilizunguka wilaya za Bukoba vijijini, Karagwe, Ngara, Biharamulo na Muleba wakihubiri habari njema ya wokovu na kuonyesha sinema ya maisha ya Bwana wetu Yesu Kristo.

Mwaka 2004ulifanyika uinjilisti katika maeneo mbali mbali ya wilaya ya Karagwe na wengi walitoa maisha yao kwa Bwana Yesu.

Tena mwaka 2005, 2006, 2007, 2008, 2009 injili imehubiriwa kwenye vijiji vya Kyegolomola, Bushasha-Bugabo, na Kaibanja, na imeshuhudiwa watu wengi sana wakitubu dhambi zao na kumrudia Bwana Yesu bila kujali mipaka yao ya dini au madhehebu. Pia tulishuhudia Bwana Yesu akiponya na kuwafungua wengi waliokuwa wakisumbuliwa na magonjwa na nguvu za giza. Na hata katika maeneo mengine tulishuhudia watumishi wa Mungu wa maeneo hayo waliokuwa hawashirikiani kwa sababu ya hali ya kidhehebu wakishirikiana tena katika kumtumikia Bwana pamoja.

Pia injili imehubiriwa katika shule za sekondari za Nyakato, Ihungo, Bukoba, na Kagemu.

Tunaendelea kupokea ushuhuda jinsi watu wengi waliookoka katika kampeni hizi wanavyoendelea vizuri katika Bwana, na hii inatutia moyo.

SHIRIKI KATIKA BARAKA ZA HUDUMA HII:

Inafurahisha kwamba tayari tumeshaanza kupokea mialiko kutoka maeneo mbalimbali tuliyoyatembelea na kuhubiri injili mwaka iliyopita. Na sasa tunahitaji kutembelea maeneo mengine zaidi mwaka huu. Hata hivyo tunahitaji msaada wako ili tuweze kufika katika maeneo hayo na maeneo mengine mapya. Tunahitaji kuungana na wewe katika kuhubiri injili katika maeneo haya na wewe unaweza kuwa sehemu ya wahubiri hao hata kama binafsi hukufika katika maeneo hayo, kwa kutuchangia na michango yako itakuwa baraka kabisa katika huduma hii. Tuna uhakika baraka zitakazopatikana na wewe binfsi utahusika kuzipata. Ebu tuchangie katika huduma hii kwa kutuandikia ukitumia mawasiliano haya.

KUOKOKA:

Je na wewe unataka kuokoka? basi ebu tuandikie kwa kutumia anuani yetu iliyo katika ukurasa wa Kwanza au tutumie email kupitia rhematz@rhematanzania.org na andika katika kichwa cha habari kwamba NATAKA KUOKOKA tuambie jina lako na mahali uliko na sisi tutakuombea na kukupa msaada wa kila namna ili umpokee Bwana Yesu naye awe Bwana na mwokozi wa maisha yako.

Na unaweza kuokoka leo kama unapenda kumpa Yesu maisha yako ( Matendo ya Mitume 17:30 "Basi zamani zile za ujinga Mungu alijifanya kama vile azioni; bali sasa anawaangiza watu wote wa kila mahali watubu."na 16: 30-31 "....... yanipasa nifanye nini nipate kuokoka? Wakamwambia mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako"). Basi kama uko tayari kuokoka leo, unaweza kuomba sala hii hapa chini kwa sauti na huku ukiamini ndani ya moyo wako kwamba unayoomba ndiyo yaliyo katika kusudi la moyo wako:-

BWANA YESU NAFUNGUA MLANGO WA MOYO WANGU NA NAJITAMBUA KWAMBA MIMI NI MWENYE DHAMBI. NINAHITAJI MSAADA WAKO. NAHITAJI KUSAMEHEWA DHAMBI ZANGU ZOTE, NINAZO ZIJUA NA NISIZO ZIKUMBUKA. NINATUBU MBELE ZAKO KWAMBA SIHITAJI TENA KUISHI KATIKA MAISHA YA DHAMBI NA SITAENDELEA KUKUASI NA KUMTUMIKIA SHETANI. NIFUTE KATIKA KITABU CHA HUKUMU NA NIANDIKE UPYA KATIKA KITABU CHA UZIMA WAKO. ASANTE YESU KWA KUNISAMEHE. ASANTE YESU KWA KUNIOKOA. AMEN."

Basi kama umeomba sala hii kutoka ndani ya moyo wako (Warumi 10:8-10 ".....Kwa sababu ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka.....") Tuandikie barua kwa anuani iliyo katika ukurasa wa kwanza au bonyeza hapa kupata mawasiliano na pia unaweza kupiga simu namba +255 713 095 111 au +255 754 771 552 na kutuambia jina lako na mahali ulipo ili tuendelee kukuombea, kukufundisha na kukutia moyo katika safari mpya na maisha mapya. Tunahitaji kuona unasogea mbele kiroho hivyo usisite kutuandikia na kutuelezea kuhusu uamuzi wako huu mpya.

Tafadhali tembelea kurasa zingine katika tovuti hii uweze kupata msaada zaidi!

 

RUDI UKURASA WA KWANZA

RUDI MWANZO WA UKURASA HUU