USHIRIKA WA PAMOJA (UNITY CHRISTIAN FELLOWSHIP.)

Hii ni huduma mama katika Rhema Outreach Ministries inayowaleta Watu waliookoka, kutokea maeneo mbalimbali  na katika madhehebu mbalimbali ambao wameamua kukaa pamoja kwa umoja na kujifunza kumtumikia Mungu pamoja bila ya kujali mipaka ya itikadi (doctrine) zao za kidini wala mipaka ya makanisa yao. Wanachojua ni kimoja tu! kwamba wao ni mwili wa Kristo. Wao ni kanisa la Bwana.

Wanaushirika hawa wameamua kujifunza kuishi kama kanisa la kwanza Matendo 2:44-47.

Ni kutoka katika huduma hii ya Unity Christian Fellowship ambapo huduma zote za Rhema Outreach zimezaliwa.

Huduma hii inafanyika kupitia katika muundo wa mitaa.
Katika kila mtaa una kiongozi anayesimamia huduma zote za kichungaji katika eneo la mtaa wake: uwajibika katika mtaa huo kufundisha na kuhakikisha maisha ya kiroho ya wanaushirika (wana fellowship) yanaendelea vizuri na wanaishi maisha mazuri kama neno la Mungu linavyomtaka kila mkristo aishi. Yeye huelekeza na kufundisha. Pia ni jukumu lake kiongozi kulea vipawa vya washirika wake. Watu wote walio katika eneo hili (mtaa) hukusanyika katika mojawapo ya nyumba zao katika siku wanazopanga katikati ya wiki kujifunza, kuomba, kushuhudia na kupanga mipango mbalimbali inayohusiana na huduma katika eneo lao. Mitaa mingine ufanya hata ibada za usiku pamoja.

Na kutokana na mitaa, tena tunapata ushirika wa pamoja (unity fellowship). Hii ni pale  watu wote waliookoka kutokea katika mitaa yote wanapokutana pamoja katika eneo walilokubaliana (kwa sasa wanakutana kwenye ukumbi wa unity Christian fellowship uliopo katika eneo la miembeni karibu na ukumbi wa St Francis Bukoba mjini) ili Kujifunza neno la Mungu, Kuomba pamoja, kufanya huduma mbalimbali zinazoliinua jina la Bwana Yesu pamoja, na kuwaleta watu mbalimbali kwa Bwana Yesu katika mji wa Bukoba.

Kila siku ya Jumapili jioni kuanzia saa 8 hadi saa 12 huwa kuna kusanyiko la pamoja la watu kiasi cha 200 hadi 300 ambao hukutana kwa wakati mmoja kujifunza. Wakati wa asubuhi washiriki wa fellowship wanaokwenda katika ibada za madhehebu yao wana uhuru wa kufanya hivyo.

Pia tumeshudia baraka nyingi kupitia kusanyiko hili maana kadri ya wastani wa watu 5 humpokea Bwana Yesu kila Jumapili tukutanapo. Jambo hili limewaletea nuru ya Bwana wetu Yesu Kristo wengi.

Na tena kupitia maombezi yanayofanyika katika huduma hii, watu wengi wamefunguliwa shida mbalimbali ikiwemo magonjwa na mapepo na kila aina ya vifungo na mateso. Tazama ukurasa wa shuhuda

Huduma imekuwa ikitoa mafundisho ya maisha ya ukristo kwa makundi maalum ya vijana, watoto, watu walio katika ndoa na wajane.

Moja ya maono ya huduma hii hivi sasa ni kuzalisha watumishi (watenda kazi). Na kwa sababu hiyo masomo maalum ya ufuasi na uanafunzi yanatolewa ili kila mshirika ahusike katika kufanya yale anayotakiwa kuyafanya katika kuujenga ufalme wa Mungu. Kila mmoja anatakiwa kuendelea kutumia karama aliyopewa katika kuujenga mwili wa Kristo.

Unaweza kuagiza DVD za video za mafundisho ya kila wiki kwa bei ya shs. 5,000/= tu. Tuandikie kwa mawasiliano yaliyowekwa hapa ukibainisha mahitaji yako na anuani yako ya posta, tutakutumia.

 

 

RUDI UKURASA WA KWANZA

RUDI MWANZO WA UKURASA HUU

"1 Petro 1:22" Mkiisha kujitakasa roho zenu kwa kuitii kweli, hata kuufikilia upendano wa ndugu usio na unafiki, basi jitahidini kupendana kwa moyo."