UTAMBULISHO:

"Je laweza neno jema kutokea Nazareti?"Kama vile Nazareth ulivyokuwa machoni pa wayahudi wengi mji uliodharaulika; Bukoba pia umekuwa mji duni machoni pa wengi. Hii ni kutokana na mfululizo wa majanga kama ukimwi uliojitokeza kwa mara ya kwanza Tanzania katika mji huu mwaka 1983, historia mbaya ya ugonjwa wa Syphilis, wakina mama waliosambaa Afrika mashariki miaka ya 60 katika biashara ya umalaya, vita ya Idd Amini 1978, ajali mbaya ya meli 1996 na mengine mengi. Hata hivyo wengi wasilojua ni historia ya uamsho uliopita kama mafuriko miaka ya ’30 kwa zaidi ya miaka 50. Uamsho huu ulioitwa uamsho wa Utakatifu kwa vile ulivyosisitiza juu ya toba na kutengeneza maisha na kutembea katika nuru ulianzia Rwanda wakati watu wawili waliokuwa wanasali pamoja lakini wakiwa na uhasama kati yao walipokutana ghafla sehemu waliyokuwa hawategemei na ikawa vigumu kwao kukwepana. Ndipo Roho Mtakatifu alipowabana na badala ya kugombana waliangukiana na kutubu kila mtu kwa mwenzake. Waliosikia habari ya maadui hawa walielewana kwa muujiza ndipo nao waliguswa na Mungu na kuanza kutubu dhambi zao waliofanya hata kama walikuwa makanisani. Uamsho huu ulipitia Uganda na kuingia katika mkoa wa Kagera. Upendo wa kweli kati ya ndugu ulikuwa ni tabia ya uamsho huu. Ndipo shetani alinyanyuka kujaribu kufuta kabisa baraka za uamsho huu kwa udini, uharibifu na majanga. Lakini habari njema ni hii "Karama za Mungu hazina majuto....."

Ingawa katika mji huu kuzimu imefungua kinywa kutema uharibifu na kumeza mema yaliyopata kutokea hapa; kusudi la Mungu ndilo litakalosimama. Mungu amekusudia tokea katika mji huu kuufunga mlango wa kuzimu na kufungua hapa madirisha ya mbinguni. Bukoba utakuwa mji utaokampa Mungu utukufu katika viwango vikuu katika hizi siku za mwisho. Kutoka hapa heshima ya Mungu itakuwa kubwa na wengi katika Tanzania, Afrika na dunia nzima watabarikiwa. Watakunywa maji ya chemchem ya Bukoba na kuburudishwa wakitiwa moyo na wengi kumgeukia Mungu. Ee Bukoba lisikie neno la Bwana "Kwa kitambo kidogo nimekuacha; lakini kwa rehema nyingi nitakukusanya. Kwa ghadhabu ifurikayo nalikuficha uso wangu dakika moja lakini kwa rehema nyingi nitakukusanya." Mungu amekuwa akisema na kanisa la Bukoba katika miaka ya karibuni juu ya uamsho mkubwa ulio mbele yetu. Katika hali hii Mungu alituongoza mwishoni mwa miaka ya 1990 kujiandaa kwa ajili ya jambo jipya Mungu analofanya. Wakati Mungu alipoanza kuzungumza nasi juu ya jambo hili alisisitiza juu ya mvinyo mpya inayohitaji viriba vipya. Tuanaamini kuwa Mungu anaunda viriba vipya katika siku zetu.

Tulihimizwa rohoni kuanza huduma hii isiyo na mipaka ya kidhehebu au kidini. Huduma itakayoshirikiana na madhehebu yote ya dini bila ubaguzi. Tuliletwa pamoja kama familia na kule kuzaliwa mara ya pili kwa uwezo wa Roho Mtakatifu yaani Wokovu (maisha mapya ndani ya Kristo), ili tuzishike kweli za kibiblia (Neno la Mungu), na kiu ya kuishi kwa kuyatii maagizo ya biblia katika kumwishia Mungu.

Historia fupi ya huduma hii inaanzia mwaka 1994 pale mwanzilishi wake ndugu Johannes Kasimbazi alipopata maono ya kuanzisha huduma itakayowafikia watu mbalimbali kwa neno la Mungu na kuwajenga katika hali ya umoja ndani ya mwili wa Kristo na kuleta uamsho bila kuzuiwa na vizingiti vya misimamo, desturi za kidhehebu na kidini. Ndipo huduma hii ikaanza kama timu ya maombi katika mji wa Bukoba. Mzigo wetu ukiwa kuombea nchi na mkoa wa Kagera. Muda mfupi baadaye watu waliongezeka na ikawepo haja ya kufundisha mambo ya msingi katika maisha ya wokovu pamoja na jinsi ya kuomba. Hadi sasa katika sehemu mbali mbali tungali tunasisitiza na kufundisha hayo. Wakati huu tunayo matawi sehemu mbali mbali za Tanzania kama Kibaha, Dar es salaam na Bukoba.

Fahamu ya kuwa unaposoma tovuti hii Mungu anakusudia kukufanya sehemu ya makusudi yake katika nyakati hizi za mavuno makubwa. Mungu akubariki.

Nduguyo katika utumishi,

Florence na Johannes Kasimbazi.

 

 

 

RUDI UKURASA WA KWANZA

RUDI MWANZO WA UKURASA HUU